Wananchi mkoani Singida wametakiwa kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu ili kuweza kuutokomeza na kuwa na afya bora ambapo imeelezwa kuwa mwaka 2021 walingundulika wagonjwa wapya 2597 na mwaka 2022 wagonjwa 2724 sawa na asilimia 93.19 ya lengo la ugunduzi wa wagonjwa 2923 ambalo Mkoa ulipewa na Mpango wa Taifa wa kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI).
Wito huo umetolewa leo na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Thomas Apson, wakati akisoma hotuba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba katika maadhimisho ya siku ya Kifua Kikuu duniani yaliyofanyika kimkoa kijiji cha Ilongero Halmashauri ya Wilaya ya Singida.
DC Apson amesema ugonjwa wa Kifua Kikuu bado ni changamoto la kijamii hivyo kuna umuhimu wa kuchukua hatua madhubuti katika mapambano dhidi yake huku akifafanua kuwa endapo jamii itahusika kikamilifu katika mapambano hayo ugonjwa huo utakwisha.
Aidha DC amefafanua kuwa takwimu hizo zinamaanisha kwamba katika kila watu mia moja (100) watu ishirini na moja (21) wanaugua Kifua Kikuu ndio maana jamii inahitajika kutilia mkazo hamasa ya kupambana na ugonjwa huu na namna ya kujikinga.
Akiendelea na hotuba yake amesema katika kuadhimisha siku ya Kifua Kikuu duniani wananchi wa Mkoa wa Singida wanapaswa kuelewa na kuzingatia kuwa ugonjwa huo unasababishwa na bakteria na huenezwa kwa njia ya hewa kutoka kwa mgonjwa ambaye hajaanza matibabu na siyo kwa kulogwa wala kurithi kama inavyoaminika kwa baadhi ya watu.
Pia amesisitiza kuwa uchunguzi wa tiba ya Kifua Kikuu hufanyika bila malipo katika Vituo vya Huduma za Afya vya Serikali na Bisafsi hivyo jamii imehaswa kutokuwa na hofu ya gharama wala woga wa kwenda hospitali kwaajili ya kupima na kupatiwa matibabu.
Mkuu huyo wa Wilaya amewahimiza wananchi wa mkoa huo kuhakikisha kuwa nyumba wanazoishi zina mzunguko wa hewa na mwanga wa jua wa kutosha ili kuepusha maambukizo ya Kifua Kikuu.
Ameeleza kuwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano (5) wanaoishi kwenye kaya yenye mgonjwa wa Kifua Kikuu wanatakiwa kufanya uchunguzi mapema kwani wapo katika hatari ya kuambukizwa. Pia ni muhimu kwa wazazi au walezi kuwapa taarifa walimu wa afya au walezi wa shule kuhusu matibabu ya Kifua Kikuu ya watoto wao.
“Kumbuka si kila mgonjwa wa Kifua Kikuu ana VVU na si kila anayeishi na VVU ana Kifua Kikuu. Chukua hatua, kapime afya” Amesisitiza Dc Apson
Akizungumzia kuhusu lishe kwa mgonjwa wa Kifua Kikuu Dc Apson, amesisitiza kuwa mgonjwa huyo anahitaji kupatiwa lishe bora ili kuimarisha afya yake pamoja na kupata ushauri kuhusu lishe kutoka kwa mtoa huduma.
“Kifua Kikuu kinatibika na kupona kabisa; hivyo kuacha kunywa dawa za Kifua Kikuu kikamilifu kunaweza kusababisha vimelea kuwa sugu na hivyo kuambukiza Kifua Kikuu sugu watu wa karibu yako”. Amefafanua DC Apson
Maadhimisho ya siku ya Kifua Kikuu duniani huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 24 mwezi Machi. Kauli mbiu; KWA PAMOJA TUNAWEZA KUTOKOMEZA KIFUA KIKUU NCHINI TANZANIA.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.