Katibu Tawala Mkoa wa Singida Mwl. Dorothy Mwaluko amekutana na Wakuu wa shule za Sekondari na wadau wengine wa Mkoani hapo, kujadili namna ya kuboresha Mazingira ya utoaji wa elimu katika shule hizo ili yawe rafiki kwa walimu na wanafunzi.
Akiongea katika Mkutano huo uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa VETA uliopo Singida Mjini, Katibu Tawala amesema, Serikali itaboresha elimu ya Sekondari kwa kuangalia uboreshaji wa majengo, huduma muhimu mashuleni na upatikanaji wa chakula ili kuongeza viwango vya ufaulu.
Amesema ili kuimarisha taaluma Mkoani hapo ni lazima kuwepo kwa vifaa stahiki vya kufundishia na kujifunzia, mafunzo kwa walimu, matumizi ya TEHAMA na uwepo wa masomo muda wa ziada kwa wanafunzi.
Aidha, amebainisha kwamba ili Mkoa uweze kufanikiwa Katika kuinua viwango vya elimu ni lazima kuwepo na uwajibikaji na ushirikishwaji baina ya walimu, wanafunzi, wazazi na jamii kwa ujumla ambapo viongozi au wasimamizi wataimarisha ufuatiliaji, nidhamu na maadili.
Mwaluko amewataka wakuu wa shule kuongeza ubunifu huku akieleza mpango wa kuweka viashiria vya kuwapima ufanisi wakuu hao kwa kuangalia mahudhurio ya walimu na wanafunzi yasiwe chini ya asilimia 80 mpaka 95, taarifa ya mwalimu wa zamu ya kila siku, daftari la mahudhurio la walimu na daftari la mahudhurio la wanafunzi kwa kila darasa.
Hata hivyo Mwaluko ameeleza kwamba Serikali inaendelea na Mpango wake wa kuhakikisha kwamba kila shule inakuwa na vifaa vya kufundishia vikiwemo vitabu, maabara na shajara na uwepo wa mafunzo kazini ya walimu.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.