Maendeleo ni hali ya kuwa na mabadiliko kutoka hatua moja hadi nyingine, kwa lengo la kuyafikia mafanikio yaliyokusudiwa na jamii husika, kama vile sekta ya elimu, afya na miundombinu, kwa nia thabiti ya kurahisisha maisha.
Hali hiyo humwezesha mtu mmoja mmoja, familia na vikundi kupata mabadiliko chanya, baada ya kuongeza maarifa kupitia ujuzi, ambao baadaye huwanyanyua kiuchumi, kupitia kazi halali, kulingana na mbinu kabambe, zilizoandaliwa mahususi ili kusukuma gurudumu hilo.
Katika nchi yetu ya Tanzania anayesimamia jukumu hilo ni mwanamke hodari na mchapa kazi, Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa awamu ya sita, wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyekusudia kwa dhati kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii ya maendeleo, kwa Taifa lake.
Kama ambavyo mataifa mengi Duniani, yamethibitisha uwezo wa kiuongozi wa mwanamke huyu kwa miaka mitatu ya utawala wake, ndivyo Watanzania wamejionea mabadiliko chanya ya maendeleo, kupitia sekta mbalimbali.
Kwa kudhihirisha hilo, utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi mkuu mwaka 2020-2025, Mkoani Singida, umetekelezwa na serikali ya awamu ya sita, kwa ufanisi na umahiri mkubwa, katika miradi kadha wa kadha ya maendeleo.
Serikali Mkoani Singida, imesema miaka mitatu ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, katika Mkoa huo, yameonekana mabadiliko makubwa ya maendeleo, kupitia sekta mbalimbali, jambo linalopaswa kuungwa mkono na wananchi wote.
Mkoa wa Singida umepokea jumla ya Sh. 660,328,310,459.77, sawa na ongezeko la asilimia 432, kutoka kiasi cha Sh. 124,046,314,164.00, zilizopokelewa kipindi cha mwaka wa fedha 2019/20 na 2020/21.
Kiasi hicho kikiwa ni mapato kutoka Serikali Kuu, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wadau mbalimbali wa Maendeleo na Wananchi kwa ujumla, hali iliyosbabisha kuwepo kwa mafanikio makubwa katika Sekta mbalimbali.
Wananchi wa Mkoa wa Singida, wanamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa, kwa kweli anayoendelea kuifanya hususan katika mambo makubwa, kwa kutuletea maendeleo.
SEKTA YA AFYA, USTAWI WA JAMII NA LISHE
Katika sekta ya afya kwa miaka mitatu ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Mkoa wa Singida umeboresha upatikanaji wa huduma bora za afya katika ambapo huduma imeimarika mwaka hadi mwaka ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.
Katika kutekeleza Sera ya kusogeza huduma kwa Wananchi miundombinu ya afya iliyojengwa na kukamilishwa, imewezesha watu wa Singida kuwa na uhakika wa matibabu, kutokana na Sh. 56,571,619,921.51 kutekeleza miradi na shughuli mbalimbali katika sekta ya afya.
Baadhi ya shughuli hizo amezitaja kuwa ni, ujenzi wa Hospitali nne mpya, kwenye Wilaya za Mkalama, Itigi, Ikungi na Singida, ujenzi wa vituo vya afya 22 na ukamilishaji wa zahanati 69.
Huku maeneeleo mengine yakiwa ni, kukamilisha ujenzi wa majengo manne ya dharura (EMD), majengo matatu kwa ajili ya wagonjwa mahututi (ICU), na ujenzi wa nyumba sita (3 in 1) za makazi ya watumishi wa Afya. Manunuzi ya vifaa tiba na dawa katika hospitali saba za Wilaya, Vituo vya Afya 22 na zahanati 220, ujenzi wa miundombinu na ununuzi wa vifaa tiba kwenye hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida, na ukarabati wa hospitali kongwe za Singida Manispaa, Manyoni na Iramba.
Katika ibara ya 84 ya Ilani ya uchaguzi, inaielekeza wazi juu ya sekta ya afya, kuimarisha mfumo wa bima ya afya, ikiwemo mifuko ya bima (NHIF na CHF) na huduma bila malipo, kwa afya ya mama na mtoto ili kupunguza vifo kwa wajawazito na watoto walio na umri chini ya miaka mitano, jambo hilo limetekelezwa kwa kiwango kikubwa.
Anabainisha kuwa, miundombinu ya Afya kupitia Hospitali, Vituo vya Afya, Zahanati, Vyuo vya Mafunzo na Vituo vingine vya kutolea huduma za Afya, vimeongezeka, kutoka 259 mwaka 2022 hadi 350 kufikia Disemba, 2023, hivyo lazima pongezi kubwa zielekezwe kwa Mhe. Rais.
Aidha, kuimarika kwa miundombinu ya Afya kwa ngazi ya Hospitali, Vituo vya Afya, Zahanati, Vyuo vya Mafunzo; kumeongeza Vituo vya kutolea huduma za Afya kutoka 259 mwaka 2022 hadi kufikia 350 Desemba, 2023.
Baada ya wananchi kujengewa miundombinu ya afya karibu na maeneo yao, hivi sasa wananufaika na huduma za upasuaji wa dharura, kupitia vituo 21 (zikiwemo hospitali 11 na vituo vya Afya 10), hivyo kuondoa kabisa changamoto ya kusafiri umbali mrefu, kwa ajili ya kufuata matibabu.
HALI YA UCHUMI WA MKOA
Serikali ya awamu ya sita imehakikisha asilimia 80 ya wananchi wa Mkoa wa Singida wanaojihusisha na kilimo (kilimo, ufugaji na, Uvuvi), wanapata mafanikio na kukua kwa pato la Mkoa, kutoka Sh.Trilioni 2.8 mwaka 2020 hadi kufikia Sh. Trilioni 3.0 mwaka 2021.
Kukua kwa pato la wastani la kila mtu katika Mkoa wa Singida, kutoka Sh. 1,651,785 mwaka 2020 hadi kufikia Sh. 1,721,195, mwaka 2021.
Hali ya utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini, Rais ameupatia Mkoa wa Singida zaidi ya Sh. 7,014,866,722, zilizolipwa kama ruzuku kwa walengwa katika Vijiji na Mitaa 512 katika Mkoa wa Singida.
Huku bajeti ya mapato ya ndani ya Mkoa ikiongezeka kutoka Sh. 19,020,096,000 mwaka 2022/2023 hadi kufikia Sh. 20,046,140,350.00, kwa mwaka 2023/2024.
MCHANGO WA KILIMO KWA PATO LA MKOA
Mkoa wa Singida, katika kipindi cha miaka mitatu Sekta ya uchumi na uzalishaji imepokea fedha shilingi 44,386,715,280.00 kwa ajili ya kutekeleza shughuli za maendeleo na kupata mafanikio mbalimbali.
Baadhi ya mafanikio hayo ni, serikali kusambaza tani 2,973 za mbolea ya ruzuku kwa wakulima 8,342 na tani 863.004 ya mbegu za alizeti kwa bei ya ruzuku. Kumekuwepo na kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya chakula, biashara, mbogamboga na matunda, kutoka tani 1,120,566 msimu wa 2021/22, hadi kufikia tani 1,507,226.9 sawa na asilimia 74.3 kwa msimu wa mwaka 2022/23.
Hali kadhalika kutokana na kipaumbele kwa zao la alizeti, uzalishaji umeongezeka kutoka tani 145,915.8 mwaka 2021/22, hadi 311,318.38, mwaka 2022/23, kutokana na Serikali kutoa ruzuku ya mbegu kwa wakulima.
UJENZI WA MIRADI YA UMWAGILIAJI
Serikali ya awamu ya sita imeendelea na ujenzi wa bwawa la skimu ya umwagiliaji yenye ukubwa wa ekari 2,000, katika Kijiji cha Msingi, Wilaya ya Mkalama, na itagharimu Sh. 34,176,081,080.00 hadi kukamilika kwake, huku tayari Sh. 5,200,000,000.00, zikiwa zimetumika kwenye mradi huo.
Mradi huo utanufaisha zaidi ya wananachi 12,000, kutoka Vijiji vinne vya Ishinsi, Kidi, Ndurumo na Msingi, katika Wilaya ya Mkalama na maeneo jirani, ndani ya Mkoa wa Singida.
Hata hivyo katika miaka mitatu chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan, tayari kuna maeneo mengine 92 yametambuliwa ndani ya Mkoa, kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, kati ya hayo maeneo 38 ni skimu, zikiwemo 19 zilizoendelezwa na zingine 19 zikiandaliwa, kuhimili kilimo cha umwagiliaji.
SEKTA YA MIFUGO
Serikali ya awamu ya sita, imeboresha sekta ya mifugo na hadi kufikia Desemba 2023, kulikuwa na ng`ombe 1,240,853, mbuzi 740,210, kondoo 312,940, nguruwe 18,826, punda 26,692, mbwa 68,740 na kuku 2,684,382. Kwa msimu wa 2022/23, jamii ilijipatia kiasi cha Sh.1,661,365,547.89, sawa na asilimia 11.9
Hata hivyo Serikali ya Mkoa wa Singida imefafanua kuwa mapato yatokanayo na sekta ya mifugo kwa nusu mwaka pekee, yalikuwa Sh. 918,541,106.86, kuanzia kipindi cha Julai hadi Desemba, 2023.
SEKTA YA MAJI
Katika kuhakikisha jamii inanufaika na huduma ya maji safi na salama, kiasi cha Sh. 3,962,434,442.37 kilitolewa na serikali kwa ajili ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Singida (SUWASA), kutekeleza miradi ya maji.
Kiasi hicho kimeleta mabadiliko makubwa ya upatikanaji wa maji ya kutosha kati ya machi 2021 hadi Januari 2024, kwa uzalishaji kuongezeka kwa lita 2,967,000, kutoka wastani wa lita 8,500,000 kwa siku hadi lita 11,467,000. Mtandao wa usambazaji maji umeongezeka kwa kilomita 59.6 kutoka kilomita 341.45 hadi kilomita 401.1 na wateja wa maji safi wakiongezeka kutoka 14,025 hadi 19,819.
Upatikanaji wa maji safi umeongezeko kutoka asilimia 58 hadi kufikia 85, katika halmashauri ya Manispaa ya Singida, huku hali halisi ya upatikanaji wa huduma hiyo kwenye miji midogo ya Ikungi, Puma, Iguguno, Makiungu, Sepuka, Irisya na Njiapanda, ikifikia asilimia 65.
Hata hivyo anasema, ujenzi wa mabwawa matano ya kutibu maji taka na baadaye kujenga mitandao ya mabomba ya kukusanyia maji taka katika Manispaa ya Singida, inaendelea na tayari umeshatekelezwa kwa asilimia 34.
Kuhusu ujenzi wa miundombinu ya Maji katika Manispaa ya Singida, kupitia mradi wa Miji 28 kwa gharama ya USD 17,718,757, sawa na kiasi cha Sh. 42,000,000,000 za Tanzania, unaendelea vyema, kwa shughuli za kutafiti vyanzo vya maji, chini ya ardhi.
Kuhusu upatikanaji wa maji katika mji wa Manyoni, kiasi cha Shilingi 29,084,673,818.577, kikihusisha mapato ya ndani na ruzuku ya serikali kuu zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji kwa kipindi cha miaka mitatu na kuongeza uzalishaji wa maji kutoka wastani wa lita 1,672,166 hadi 2,057,000 na hivyo kuongeza wateja kutoka 2,429 hadi 4,707.
Kadhalika upatikanaji wa majisafi umeongezeka kutoka asilimia 51 mwaka 2020/2021 hadi 78 mwaka 2023/2024 katika mji wa Manyoni na Itigi, huku ili kuhakikisha tatizo hilo linaisha kabisa, kuna ujenzi wa miundombinu ya Maji Manyoni kupitia mradi wa Miji 28 (USD 10,584,823), sawa na Sh. 25,089,936,309.687 unatekelezwa.
Miaka mitatu ya Dk. Samia Sukluhu Hassan katika Wilaya ya Iramba, kiasi cha Sh. 30,665,765,594.049 kimepekewa kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji katika mji wa Kiomboi, ambao ni makao makuu ya Wilaya.
Na kupitia Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), umeboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji Vijijini kwa Mkoa wa Singida kutoka asilimia 57.9 mwaka 2020/2021 hadi kufikia asilimia 67.7 Januari, 2024 sawa na wakazi 1,109,220 kati ya 1,636,735 wanaoishi Vijijini.
Jumla ya Vijiji 265 vinapata huduma ya maji safi na salama, kupitia mitandao ya mabomba, na Vijiji vingine 124 vinapata huduma hiyo kupitia visima vifupi.
Aidha, Mkoa umepokea Sh. 31,840,921,775.26 katika kipindi cha kuanzia Machi 2021 hadi kufikia sasa, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji Vijijini na hivyo kusababisha mabadiliko chanya kwa jamii ya Singida.
BARABARA (TANROADS)
Serikali imeweza kutoa Sh. 221,582,532,996.69 kwa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Singida anayehudumia Km 1,718.31 za barabara kuu na za Mkoa, kati ya hizo zikiwemo Km.490.30 ni barabara za lami, sawa na asilimia 28.5, na sehemu iliyobaki ya km 1,228.01 ni barabara za changarawe, ikiwa ni sawa na asilimia 71.5.
Kiwango hicho cha fedhaa kimefanikisha ujenzi wa miradi mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa kivuko cha watembea kwa miguu (Under pass), katika Mtaa wa Kibaoni, barabara ya Kintinku- Singida- Malendi, na tayari kimekamilika.
MIRADI YA USANIFU KITAIFA
Kazi ya usanifu wa kina kwa ajili ya Ukarabati wa barabara ya Shelui-Nzega, Km 123, ambako Mkoa wa Singida una jumla ya Km 17 na ukarabati wa barabara ya Singida-Shelui (km110) kazi ya usanifu inaendelea.
Ujenzi wa barabara ya Sabasaba-Sepuka-Ndago-Kizaga (Km77.6) kwa kiwango cha lami, tayari usanifu umefanyika na mkandarasi amekabidhiwa eneo, huku barabara ya Singida Urban-Ilongero hadi Haydom (Km93.3) na Ikungi-Londoni hadi Kilimatinde (Solya) Km117.8, kwa kiwango cha lami usanifu umekamilika kwa asilimia 90.
WAKALA WA BARABARA ZA VIJIJINI NA MIJINI (TARURA)
Kipindi cha Machi 2021 hadi Januari, 2024, Serikali imetoa Sh. 68,279,632,343.8 kwa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), anayehudumia mtandao wa barabara wenye jumla ya urefu wa km 5,669.412, huku km 1,946.08 zikiwa ni barabara za Makusanyo (Collector roads), km 2840.62 ni barabara za mlisho (Feeder roads) na km 863.20 ni barabara za jamii (Community roads).
Kutokana na kiasi hicho cha fedha, mtandao wa barabara za lami umeongezeka kutoka Km 29.8 hadi kufikia Km 43.9, sawa na ongezeko la Km 14.1. huku mtandao wa barabara za changarawe ukiongezeka kutoka Km 968.97 hadi kufikia Km 1,512.52, ikiwa ni ongezeko la Km 543.55.
Aidha mtandao wa barabara za udongo hivi sasa zimepungua Mkoani Singida, kutoka Km 4,670.37 hadi kufikia Km 4112.63. wakati jumla ya madaraja ama vivuko 794, tayari vimejengwa katika maeneo mbalimbali ya barabara zinazosimamiwa na TARURA.
SEKTA YA NISHATI NA UMEME (TANESCO)
Katika Utekelezaji wa ilani ya mwaka 2020-2025 katika Ibara ya 18 inatoa maelekezo kwa sekta za uchumi na uzalishaji kuongeza kasi ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, kwa kuendelea kujenga na kuimarisha miundombinu na huduma muhimu na wezeshi zikiwemo maji na nishati.
Mkoa umepokea Sh. 118,521,720,257.59, kwa ajili ya kutekeleza miradi ya nishati ya umeme kwa kipindi cha miaka mitatu ya serikali ya awamu ya sita, na hali ya upatikanaji wa umeme ni ya kuridhisha kwa Wilaya zote.
Mpaka sasa jumla ya Vijiji 420 kati ya 441 sawa na asilimia 95.24 vimeunganishwa na umeme wa gridi ya Taifa, kutoka Vijiji 252 vilivyounganishwa hadi machi 2021, ikiwa ni ongezeko la Vijiji 158, haya yakiwa ni mafanikio makubwa.
Katika kipindi hicho, TANESCO imeweza kuunganisha umeme kwa wateja 89,623, kati yao wakiwemo wateja wakubwa wa viwanda 51, wateja wa matumizi ya kati 51,775 na wengine kwa ajili ya matumizi madogo, wakiwa ni 37,797.
Na katika kipindi hiki, TANESCO imeweza kupunguza tatizo la kukatika mara kwa mara kwa umeme, baada ya matengenezo makubwa yaliyofanywa, kutokana na kuongezeka kwa matumizi Mkoani Singida, kutoka 13.92MW mwaka 2020/2021, mpaka 19.86MW, mwaka 2023/2024.
MFUKO WA MAENDELEO YA JAMII TASAF III
Kuhusu Mpango wa serikali katika kuzinusuru kaya zilizo masikini zaidi (TASAF), unaotekelezwa katika Mkoa wa Singida kwenye halmashauri zote saba zenye mitaa 53, Vijiji 441 vyenye walengwa 57,012, waguswa wa Mpango wa TASAF.
Hadi kufikia septemba 2023, utekelezaji wa Mpango ulikuwa umefika kwenye Vijiji vyote 441 na Mitaa 53, huku walengwa wakiwa wamepokea ruzuku ya masharti na ujira wa ajira za muda, kwa fedha kiasi cha Sh, 19,547718833 zilizotolewa na serikali, kwa kipindi cha machi 2021 hadi januari, 2024.
SEKTA YA ELIMU
Kwa kipindi cha miaka mitatu ya utawala wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Serikali imejenga na kukarabati miundombinu ya elimu na kuhifadhi mazingira ya shule husika, kuimarisha misingi ya elimu ya kujitegemea katika ngazi zote, hivyo kuhakikisha mfumo mzima wa elimu unakuwa imara, kwa kuzingatia utamaduni, mila na desturi za kitanzania.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dk. Fatuma Mganga, anasema ndani ya miaka mitatu, sekta ya elimu imeimarika kwa kiwango cha juu, na hiyo imetokana na sera nzuri ya elimu bila malipo, huku kiasi cha Sh. 71,105,590,806.92 kikitumika kutekeleza kazi mbalimbali.
Kwa mujibu wa Dk. Mganga, shughuli nyingine zilizotekelezwa kipindi hicho ni ujenzi wa vyumba vya madarasa 814 katika shule shikizi na msingi, vyumba vingine vya madarasa 38, kwa elimu ya awali na madarasa mengine 617, ya shule za sekondari.
Anafafanua kuwa ujenzi wa matundu 1,866 ya vyoo kwa shule za msingi, matundu 328 kwa shule za sekondari, ukamilishaji wa vyumba vya maabara 85 ya sekondari, ujenzi wa Mabweni 48, mabwalo sita, nyumba za watumishi 65 na majengo 12 ya utawala, ni kazi zingine zilizotekelezwa ndani ya miaka mitatu ya Dk. Samia Suluhu Hassan, Mkoani Singida.
Aidha, ujenzi wa shule mpya 16 za sekondari za Kata, shule moja ya sekondari maalumu kwa wasichana, ajira ya walimu 826 wa idara ya elimu msingi na wengine 427 wa elimu sekondari, ujenzi wa shule mpya 12 za msingi kupitia BOOST, ni kati ya maeneo mengine yaliyotekelezwa na serikali ya awamu ya sita.
USAFI WA MAZINGIRA
Imeelezwa hadi kufikia Desemba, 2023, kaya zenye vyoo katika Mkoa ni asilimia 99.7, huku zile zisizokuwa na vyoo ni asilimia 0.3, wakati mahitaji ya matundu ya vyoo kwa wanafunzi wanaosoma katika shule 659 yakiwa ni 8,275 sawa na asilimia 43, huku vyoo vya walimu uhalisia ukiwa ni matundu 658, sawa na 54.
Dk. Mganga anahitimisha kwa kusema kuwa, idadi shule zenye vyanzo vya maji safi katika Mkoa wa Singida, inafikia jumla ya shule 315, kati ya 658 swa na 47.8%,
HUDUMA ZA USTAWI WA JAMII
Katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, huduma za Ustawi wa Jamii zimeimarishwa, ikiwa ni pamoja na kuwatambua Wazee na kuwapa vitambulisho vya matibabu. Aidha watoto waliopo kwenye mazingira hatarishi na makundi mengine maalumu, wakiimarishiwa huduma zao pia.
Mhe. Rais ameendelea kufanya jitihada kubwa kuhakikisha wazee wa Mkoa wa Singida, wanapatiwa huduma bora za kijamii, baada ya kuandaa utaratibu maalumu wa kulitambua kundi hilo na kupewa kipaumbele katika masuala mbalimbali, kutokana na idadi yao inayofikia watu 43,322, ambao wametambuliwa rasmi.
Miongoni mwa wazee hao, wapo wanawake 22,407 na wanaume 20,972 waliotambuliwa, huku kati yao wazee 2,852 wakiwa tayari wamepatiwa vitambulisho vya matibabu (wanaume 1,385 na wanawake 1,470, sawa na asilimia 6.5 ya wazee wenye vitambulisho, lakini zoezi la utambuzi na kuwapatia vitambulisho bado linaendelea.
Pia mabaraza ya wazee yameundwa kwa ngazi zote tangu Vijiji/mitaa 494, kata mabaraza 136, halmashauri saba na Mkoa, huku uwepo wa madirisha kwa ajili ya kundi hilo, yakiwepo kwenye vituo vyote vya kutolea huduma, sambamba na mabango yasemayo “Mpishe mzee kwanza apate huduma,” yamebandikwa.
Katika utekelezaji wa shughuli za CHF, Dk. Mganga anasema, Mkoa wa Singida una wanufaika 290,376 wenye uhakika wa kupatiwa matibabu, kupitia kadi za CHF, kwenye vituo mbalimbali vya kutolea huduma ya afya, hali inayonufaisha kwa kiwango kikubwa wananchi wenye kipato duni.
Mkoa wa Singida una jumla ya Wilaya tano, ikiwemo Wilaya ya Singida, Manyoni, Iramba, Mkalama na Ikungi, zenye halmashauri saba, ambazo ni Singida Vijijini, Singida Manispaa, Manyoni, Itigi, Mkalama, Iramba na Ikungi.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Mkoa wa Singida una idadi ya watu 2,008,058, wakiwemo wanaume 995,703 na wanawake 1,012,355, likiwemo ongezeko la watu 637,421 kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita, sawa na ongezeko la asilimia 3.8.
Serikali ya Mkoa wa Singida inampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika maeneo mbalimbali ndani ya Mkoa wa Singida kwa kipindi cha miaka mitatu (3) tangu aingie madarakani.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.