Wakulima wa Mkoa wa Singida wamedhamiria kuondoa changamoto ya uhaba wa mafuta ya kupikia ambapo Taifa limekuwa likilazimika kuagiza bidhaa hiyo nchi za nje.
Akiongea na Madiwani leo katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi na Itigi Mkuu wa Mkoa huo Peter Serukamba amesema Serikali imeendelea kuwaunga mkono wakulima wa Mkoa huo kwa kupunguza gharama za pembejeo kutoka 140,000 kwa mfuko hadi kufikia Tsh.70,000 jambo ambalo litasaidia kuongeza uzalishaji.
Amesema Mkoa wa Singida umedhamiria kuongeza eneo la kilimo kwa kupitia wadau mbalimbali wakiwemo wakulima wadogo, wakubwa, vikundi AMCOS mbalimbali vikundi vya wakulima na kupitia mashamba ya shule.
RC Serukamba ameeleza kwamba Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa hasa katika bajeti ya kilimo hivyo wakulima wa Singida wataisaidia Serikali kwa kuhakikisha wanaongeza mashamba ya alizeti, mahindi, vitunguu, mbaazi mpunga na viazi.
"Katika mkakati wa alizeti wa mwaka huu Singida tumejipanga kuhakikisha mafuta yote yaliyokuwa yakiagizwa nje ya nchi yanapaitikana Mkoani hapa, muhimu ni viongozi wa vijiji Madiwani na watendaji kuhakikisha kwamba kila Halmashauri inaongeza eneo la kilimo" alisema.
Aidha amewataka wakulima kuanza maandalizi ya Kilimo na kuhakikisha mvua za kwanza zinakuwa za kupandia ili kuondoa mazoea ya kutumia mvua za katikati ambazo mara nyingi zinakuwa hazina matokeo mazuri.
Amewahakikishia wakulima Mkoani humo kuwa Serikali itaweka Mazingira wezeshi kuhakikisha mbegu bora na mbolea zinapatikana kwa bei ya chini pamoja na masoko ya bidhaa hiyo.
RC Serukamba amefanikiwa kukutana na mabaraza ya Madiwani la Mkalama, Singida Vijijini, Manispaa, Ikungi na Itingi, hata hivyo anategemea kukutana na Madiwani wa Wilaya ya Iramba siku ya tarehe 8/9/2022 pamoja na Manyoni tarehe 10/09/2022.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.