Vyuo vya Kati vya binafsi vilivyopo Mkoa wa Singida vimetakiwa kufuata taratibu Kanuni na Sheria walizopewa wakati wa usajili ili kuondoa migogoro inayojitokeza baina yao na Watumishi ili kutoa huduma nzuri kwa wanafunzi wanaolipia fedha zao na wakufunzi wanaotoa huduma hiyo.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Binilith Mahenge alipotembelea chuo cha City Collage kilichopo maeneo ya Mwenge Mkoani hapo ambacho kimekuwa na Migogoro baina ya viongozi na Watumishi wake kwa kile kilichoelezwa kwamba ni kufanya kazi bila ya kuwa na mikataba ya kazi, kucheleweshewa mishahara yao na kutofuatwa kwa taratibu za ajira baina yao na wamiliki wa Chuo hicho.
Akiongea baada ya kupokea taarifa ya chuo hicho RC Mahenge ametoa maagizo kwa Mkuu wa chuo na Meneja kumletea ofisini kwake taarifa iliyokamilika inayoonesha miongozo waliyopewa na namna wanavyoitekeleza, na pia ioneshe makubaliano baina yao na PSF kwa ajili ya malimbikizo ya Pensheni, mikataba ya wafanyakazi na namna ambavyo wamejipanga kuondoa changamoto zilizopo chuoni hapo.
Hata hivyo Mahenge amesema ni lazima chuo hicho kiwe na Bodi ambayo itafanya kazi ambayo itasaidia kuondoa changamoto za watumishi na kuleta ushindani kwa kutoa huduma bora, huku akiwataka kuhakikisha wanakuwa na mfumo mzuri wa ajira kwa watumishi wake na kufuata taratibu zote za kiutumishi.
Aidha amekemea vikali tabia ya viongozi hao kuwatishia watumishi kuwafukuza kazi pindi wanapodai haki zao na kuwataka kufahamu kwamba madai hayo ni haki ya mtumishi hivyo kuwataka kufanya mabadiliko kabla Sheria haijachukua mkondo wake.
Akitoa taarifa ya chuo hicho Mkuu wa Chuo ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja alisema chuo kina jumla ya wanafunzi 112 na watumishi 10 ambapo wanaume ni wanane (8) na wanawake ni wawili (2) na malipo ya Ada kwa kila Mwanafunzi yakitajwa kuwa ni wastani wa Tsh laki nane (800,000/=) kwa kila Mwanafunzi.
Mkuu wa Chuo huyo anasema baadhi ya walimu wana mikataba na wengine hawana kwa kuwa bado ofisi ya Meneja inaendelea na michakato ya kuwapatia walimu waliobaki mikataba jambo ambalo lilipingwa vikali na wakufunzi wakidai mikataba hiyo imejazwa jana baada ya kusikia ujio wa Mkuu wa Mkoa.
Wakufunzi hao wamedai kufanya kazi kwa miezi minne (4) bila malipo na waliojaliwa kulipwa walikadiriwa kiasi cha kuwalipa jambo ambalo limesabisha maisha kuwa magumu huku wakipata vitisho kupitia mkuu wa shule kusimamishwa kazi kutokana na malalamiko yao kwenda Serikalini waliendelea kueleza wakufunzi hao.
Kwa upande wake kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida Jeshi Lupembe amesema kwamba chuo hicho bado kina nafasi ya kuonana na wataalamu wa Serikali katika Manispaa hiyo ili kuweza kupata miongozo mbalimbali ya kuendesha vyuo kama hivyo.
Jeshi amesistiza kufuatwa kwa taratibu hizo kwakuwa wanaoumia ni wananchi ambao watoto wao wanapata elimu isiyokidhi na kupewa vyeti visivyostahili hivyo kushindwa kuingia katika ushindani na wahitimu kutoka vyuo vingine.
Chuo hicho kinatoa kozi za TEHAMA, Malezi ya Watoto, Ufundi magari, Udereva, Utalii na Hotelia.
Kikao hicho kilihudhuriwa na wataalamu wa Halmashauri, Maafisa kazi, Wataalamu kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi wa Chuo cha vyeta Singida na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.
Mwisho
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.