Mkoa wa Singida kwa jumla una Viwanda 177 katika mgawanyo wa Viwanda vikubwa viwili (2), Viwanda vya Kati 7 na Viwanda Vidogo 168.
Mkoa wa Singida ni moja kati ya Mikoa inayotegemea zaidi usindikaji wa Mafuta ya Alizeti katika Sekta ya Viwanda. Mkoa una Viwanda 120 (vikubwa 2, vya kati 3, vidogo 115) vya kusindika mafuta ya alizeti ambavyo hutegemea malighafi inayozalishwa ndani ya Mkoa na Mikoa ya jirani.
Viwanda vyote vya kusindika Alizeti Mkoa wa Singida vina uwezo wa kusindika Tani 434,725 za Alizeti kwa mwaka wakati hali halisi ya upatikanaji wa malighafi ni wastani Tani 160,000 kwa mwaka hivyo kupelekea upunfufu wa Tani 274,725 kwa mwaka.
Mkoa una Wafanyabiashara 7,851 waliotambuliwa na Serikali kati yao wafanyabiashara 6,113 wamepewa leseni za biashara. Pia Mkoa una Masoko 37 na Magulio 81.
Mafanikio katika Sekta ya Viwanda na Biashara
Hadi sasa Wafanyabiashara 4,548 wamepata mafunzo ya uendeshaji biashara kwa nyakati tofauti yaliyokuwa yanaendeshwa na SIDO, Wakala wa Vipimo pamoja na TPSF. Wananchi 1,546 wamepewa mafunzo kuhusu usindikaji mazao. Wafanyabiashara 6,113 wametambuliwa na kupewa leseni za biashara.
Changamoto Sekta ya Viwanda na Biashara
(a) Ukosefu wa mitaji kwa wananchi katika kuanzisha viwanda vidogo
(b) Masharti magumu katika upatikanaji wa mikopo kwenye taasisi za kifedha
(c) Uingizwaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi ambazo sisi tunazalisha kwa mfano mafuta ya kula hupelekea masoko ya bidhaa zetu kushuka.
Mikakati ya kuboresha
Kuhamasisha na kutoa elimu kuhusu kilimo biashara cha alizeti ili kuongeza ufanisi.
Maandalizi ya utekelezaji wa Mkoa kufikia hali ya uchumi wa kati na viwanda
Lengo la Mkoa ni kuwa na viwanda vinavyotumia malighafi zinazozalishwa kutokana na kilimo na mifugo ambazo ndiyo shughuli kuu za kiuchumi za wananchi. Fursa zilizopo katika Mkoa ni kuanzisha na kuendeleza viwanda vya usindikaji wa alizeti, pamba, mbogamboga, ngozi, na nyama. Hii inatokana na upatikanaji wa mazao haya na hali ya hewa inayoruhusu kilimo cha mazao hayo na ufugaji.
Hali ilivyo kwa sasa
Mkoa kwa sasa una jumla ya viwanda vya kusindika alizeti 120 ambavyo kati ya hivyo viwanda viwili ni vikubwa ambapo kimoja hakijaanza kazi (Singida Grains and Oil Mill), na kimoja chenye uwezo wa kusindika tani 182,500 kwa mwaka kinafanya kazi (Mount Meru Millers).
Viwanda vya ukubwa wa kati ni 3 ambavyo vyote kwa pamoja vina uwezo wa kusindika tani 89,790 za alizeti kwa mwaka. Viwanda vidogo vidogo vipo jumla 115 na ambavyo vyote kwa pamoja vina uwezo wa kusindika alizeti tani 162,435 kwa mwaka. Hivyo, kwa ujumla viwanda vyote vina uwezo wa kusindika alizeti jumla ya tani 434,725 kwa mwaka mzima.
Katika sekta ya mifugo Mkoa una kiwanda kimoja cha kusindika ngozi ambacho ni cha ukubwa wa kati na viwanda vidogo 11 vya ngozi vinavyomilikiwa na vikundi. Mkoa umetenga eneo lenye jumla ya hekta 6,260.95 kwa ajili ya uwekezaji wa Viwanda.
Changamoto za kufikia utekelezaji wa uchumi wa viwanda
Katika utekelezaji wa uchumi wa viwanda Mkoa unakabiliwa na changamoto zifuatazo:
(a) Mfumo usio rasmi wa uuzaji wa mazao ya biashara unasababisha bei kuwa ndogo na inayotofautiana kati ya mnunuzi mmoja na mwingine na hivi kusababisha wakulima kutopata tija ya mazao yao.
(b) Matumizi hafifu ya pembejeo za kilimo kama mbegu, madawa na mbolea kunakosababishwa na bei kubwa ambayo wakulima wanashindwa kumudu
(c) Upungufu wa viwanda vya kusindika ngozi, nyama na maziwa.
(d) Miundombinu mibovu kwa baadhi ya maeneo ya uzalishaji kama vile majosho, barabara na machinjio ya kisasa.
Mikakati ya kufikia utekelezaji wa uchumi wa kati na viwanda
Ili kukabiliana na changamoto zinazokwamisha Mkoa kufikia uchumi wa viwanda, mikakati ifuatayo imepangwa kutekelezwa ifikapo 2020:-
(a) Kuhamasisha wakulima kuzalisha kwa wingi mazao ya biashara hasa vitunguu, pamba na alizeti yatakayoongeza malighafi kwenye viwanda vilivyopo na vitakavyojengwa.
(b) Kuanzisha uuzaji wa mazao kwa kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani ambao utasaidia kuwa na utaratibu mzuri wa upangaji wa bei yenye tija hivyo kushawishi wakulima wengi kulima mazao hayo.
(c) Kuelimisha wakulima umuhimu wa matumizi ya pembejeo za kilimo katika kuongeza uzalishaji kwa eneo. Lengo ni kuwafanya wakulima wajinunulie pembejeo wenyewe kwa bei ya soko kwa sababu pembejeo zinazotolewa na serikali kwa utaratibu wa ruzuku hazitoshelezi mahitaji ya wakulima wote.
(d) Kuendelea kuwahamasisha wakulima kutumia mbinu bora za uzalishaji wanazoshuriwa na wataalamu waliopo kwenye maeneo yao.
(e) Kuendelea kuwasiliana na Mamlaka husika ili kuongeza idadi ya wataalamu wa Ugani.
(f) Kukaribisha na kushawishi uwekezaji katika ujenzi wa viwanda kwa kutenga maeneo maalumu ya ujenzi wa viwanda katika Halmashauri za Wilaya ambapo jumla ya hekta 6,260.95 zimetengwa. Uwekezaji katika ujenzi wa kiwanda cha kusafisha na kufungasha vitunguu ili vipate masoko ya nje unakaribishwa sana.
(g) Kuendelea kuimarisha ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barabara vijijini, majosho na machinjio ya kisasa.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.