Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, amewataka Madaktari Bingwa waliowasili mkoani humo kuhakikisha wanatoa huduma bora, zenye heshima na utu kwa wananchi ili kuenzi taaluma yao na kuacha alama chanya katika jamii.
Akizungumza leo Oktoba 6, 2025, wakati akiwakaribisha Madaktari Bingwa wa magonjwa mbalimbali maarufu kama Madaktari wa Mama Samia, Dkt. Mganga amesema madaktari hao wamewasili Singida kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa katika Halmashauri zote saba za Mkoa huo kwa muda wa siku tano.
Amesema ni wajibu wa kila daktari kutumia ujuzi wake ipasavyo kwa moyo wa kujituma, upendo na ukarimu ili huduma watakazozitoa ziwe chachu ya matumaini kwa wananchi na kuacha kumbukumbu njema ya kazi yao.
“Tumetumwa kufanya kazi hii, hivyo yatupasa tukatumike kwa bidii, upendo na ukarimu kama fursa ya kuleta kicheko na baraka kwa wananchi tunaokwenda kuwahudumia,” alisema Dkt. Mganga.
Ameongeza kuwa utoaji wa huduma bora ni wajibu wa kitaaluma unaopaswa kuambatana na ubinadamu na moyo wa kujitolea, hasa kwa madaktari bingwa wanaokwenda kugusa maisha ya wananchi moja kwa moja. Kadhalika, ametoa wito kwa madaktari hao kuonyesha ubingwa wao kwa vitendo kwa kutoa huduma za ubora wa hali ya juu zinazolenga kupunguza idadi ya vifo vya akina mama na watoto, hususan wale waliokuwa wakisafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo katika hospitali kubwa za kitaifa kama Muhimbili.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Victorina Ludovick, amewahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kutolea huduma hizo za kibingwa ambazo sasa zimesogezwa karibu na maeneo yao.
“Huduma hizi ni za kipekee sana. Wapo wananchi wengi waliokuwa wakisafiri hadi Muhimbili au Bugando kwa ajili ya huduma kama hizi, sasa zimeletwa mlangoni mwao. Ni nafasi ya kipekee ambayo kila mwananchi anapaswa kuitumia,” alisema Dkt. Ludovick.
Ameeleza kuwa huduma zitakazotolewa ni pamoja na magonjwa ya wanawake, watoto, upasuaji, meno na kinywa, magonjwa ya ganzi na usingizi, pamoja na uvimbe, huku zaidi ya wananchi 5,000 wakitarajiwa kufikiwa katika awamu hii.
Mmoja wa Madaktari Bingwa waliowasili mkoani humo alisema kuwa timu yao imejiandaa kikamilifu kuhakikisha wananchi wa Singida wanapata huduma bora na za kibingwa kwa viwango vya juu.
“Tumewezeshwa vizuri na Serikali – tuna vifaa vya kisasa, dawa muhimu na timu kamili ya wataalamu wa fani mbalimbali. Tumejipanga kutoa huduma bora, zenye matokeo chanya kwa wananchi,” alisema mmoja wa madaktari hao.
Ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha sekta ya afya kupitia mpango huu wa Madaktari Bingwa unaolenga kufikisha huduma bora kwa wananchi katika ngazi za mikoa na halmashauri.
Uwepo wa Madaktari Bingwa mkoani Singida unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa wananchi, ikiwemo kupunguza gharama za kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za kibingwa, kuimarisha afya ya jamii kwa kugundua na kutibu magonjwa mapema, kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu afya kupitia elimu itakayotolewa sambamba na huduma, pamoja na kuongeza ujuzi kwa watumishi wa afya wa mikoa na halmashauri kupitia mafunzo ya vitendo kutoka kwa madaktari hao.
Huduma hizo za kibingwa zitaendelea kutolewa kwa muda wa siku tano katika vituo maalum vilivyopangwa kwenye halmashauri zote saba za Mkoa wa Singida, zikilenga kuboresha afya ya wananchi na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kusogeza huduma bora za afya karibu na wananchi wote.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.