Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, ameongoza maelfu ya wananchi wa mkoa huo katika mapokezi ya kihistoria ya timu ya Singida Black Stars baada ya kutwaa ubingwa wa mashindano ya CECAFA 2025, yaliyofanyika hivi karibuni.
Mapokezi hayo yamefanyika leo katika Uwanja wa Bombadia, Mjini Singida, na kuvutia maelfu ya mashabiki wa soka kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo. Furaha, nderemo na vifijo vilitawala uwanjani huku mashabiki wakiwa wamepambwa kwa jezi, bendera na mabango yenye maneno ya pongezi kwa mabingwa hao wapya wa Afrika Mashariki na Kati.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Dendego aliwapongeza wachezaji, benchi la ufundi na uongozi mzima wa Singida Black Stars kwa ushindi huo mkubwa, akisema umeiweka Singida kwenye ramani ya michezo kitaifa na kimataifa.
"Hakika timu yetu ya Singida Black Stars imebeba na kulitangaza vema jina la Mkoa. Mmetupa heshima kubwa kitaifa na kimataifa. Huu ni ushahidi kwamba Singida ni kituo kipya cha vipaji na ubora katika michezo,” alisema Mhe.Dendego kwa furaha.
Mkuu wa mkoa alisema kombe la CECAFA lina heshima kubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, na ushindi huo ni ishara ya mwanzo wa enzi mpya ya mafanikio kwa timu hiyo.
“Hizi ni salamu kwa wengine kwamba Singida Black Stars tuna jambo letu. Safari hii ya makombe ndiyo inaanza, hatuishii hapa,” alisisitiza.
Aidha, Mhe. Dendego alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuendeleza sekta ya michezo nchini, hususan kupitia ujenzi wa miundombinu na kuimarisha timu za taifa na klabu.
“Kupitia uongozi wake, tumeshuhudia miradi mikubwa ya michezo ikikamilika na hamasa kubwa kwa wachezaji wetu kushinda kimataifa – hili ndilo tunaliita Goli la Mama,” alisema Mhe. Dendego.
Akizungumzia maendeleo ya miundombinu ya michezo mkoani Singida, Dendegu alisema ujenzi wa uwanja wa mpira wa Airtel ulioko Mtipa upo katika hatua za mwisho, na mechi ya kwanza inatarajiwa kuchezwa mwezi Novemba mwaka huu.
Aidha, aliwahimiza wakazi wa Singida kuchangamkia fursa za kiuchumi zitakazotokana na uwepo wa uwanja huo, hasa katika biashara ndogo ndogo, huduma za malazi, usafiri na utalii.
“Nitoe rai kwa wawekezaji wa hoteli, wafanyabiashara na watoa huduma mbalimbali kuendelea kujipanga vema ili kunufaika na fursa hii. Uwanja huu ni baraka kwa uchumi wa Singida,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu, akisema ni wajibu wa kila Mtanzania kuchangia ustawi wa taifa kupitia sanduku la kura.
Sherehe hizo zilihitimishwa kwa burudani kutoka kwa wasanii wa ndani, maonyesho na gwaride maalum la wachezaji wa Singida Black Stars lililopamba moto uwanjani.
Ushindi huo wa CECAFA umeifanya Singida Black Stars kuandika historia mpya katika michezo ya Tanzania, na kuwa timu ya kwanza kutoka Singida kutwaa ubingwa wa kimataifa tangu kuanzishwa kwake.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.