Afya ya mtoto Mwenge aliyenusurika kifo baada ya kutumbukizwa chooni na kukaa humo kwa zaidi ya saa 14 kabla ya kuokolewa akiwa hai, inaendelea kuimarika huku akiendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Kiomboi Wilayani Iramba.
Mtoto Mwenge alitupwa chooni na mama yake mzazi Winfrida Lori (23) mwanafunzi katika Chuo cha Uuguzi cha Kiomboi Wilayani Iramba ambapo mama huyo amekiri kujifungua mtoto huyo wa kiume katika Kijiji cha Luono Julai 3, saa mbili usiku kisha kumfunga vitambaa mdomoni na kumtumbukiza chooni.
Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Kiomboi Regina Alex amesema afya ya Mtoto Mwenge inaendelea kuimarika pamoja na hali ya mama mzazi wa mtoto huyo pia inaimarika tofauti na hapo awali ambapo alikuwa dhaifu na kushindwa kumnyonyesha mtoto.
“Winifrida alikuwa hawezi kumyonyesha mtoto Mwenge hapo mwanzoni lakini sasa hivi anamnyonyesha vizuri na maziwa yanatoka ya kutosha, Mtoto mwenge ana hali nzuri na sasa amefikisha uzito wa kilogramu 2.9 hali ambayo inaridhisha kwakweli”, ameeleza muuguzi huyo.
Muuguzi Regina ameongeza kuwa licha ya mama wa mtoto Mwenge kuwa chini ya ulinzi wa jeshi la polisi, ameendelea kumhudumia mtoto wake vizuri na kwa upendo hali inayosababisha mtoto Mwenge kupata nafuu kwa uharaka.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi ambaye amempa jina mtoto huyo la Mwenge amesema kuwa jina hilo litamfutia mtoto huyo majeraha ya kutupwa chooni na kuwa ishara ya kujiamini, kujipenda, kujithamini na kumpa matumaini kama ambavyo mwenge wa huru umekuwa ukifanya.
Dkt Nchimbi amesema mwenge wa uhuru umekuwa ishara ya kuleta matumaini kwa waliokata tamaa, upendo penye chuki na heshima penye dharau na hivyo kitendo cha mama kumtupa mtoto ni kukosekana kwa amani, upendo na heshima katika maisha ya mama huyo.
Ameongeza kuwa anamtakia kila la heri mtoto Mwenge ili atakapokuwa alete heshima, upendo na amani katika maisha yake na ya wazazi wake huku akifuta kumbukumbu mbaya ya maisha yake wakati wa kuzaliwa.
Wakati huo huo Dkt Nchimbi amewaasa wazazi na walezi kuwapa majina mazuri watoto wao kwakuwa majina huwa ni sehemu muhimu ya maisha ya watoto wao na hutafsiri maisha ya baadaye.
Dkt. Nchimbi amesema jina linapaswa liwe na maono mazuri kwakuwa ndio hayo yataambatana katika maisha yake lakini jina lenye baya huleta mambo mabaya katika maisha ya mtoto.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.