Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, ametoa uhakika wa utatuzi wa mgogoro wa ardhi unaohusisha wananchi wa Wilaya ya Manyoni na Serikali, akiwataka wananchi kuwa wavumilivu na wenye subira wakati zoezi la usuluhishi na uhakiki wa maeneo ya makazi likiendelea kufanyika.

Mhe. Dendego alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na wananchi katika eneo la mradi wa ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), eneo ambalo limekuwa na mgogoro wa ardhi kati ya Serikali na wananchi wanaoishi katika maeneo yanayokusudiwa kutumika kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Mkoa alisema Serikali imejipanga kusikiliza hoja na malalamiko ya wananchi kwa kina, na kutatua mgogoro huo kwa hatua, kwa kuanza na kaya zote zilizopo katika maeneo yanayoguswa na miradi hiyo, yakiwemo maeneo ya shule za msingi na sekondari, afya, viwanda pamoja na VETA.
Alisisitiza kuwa mchakato wa utatuzi wa mgogoro huo utafanyika kwa kuzingatia misingi ya haki, uwazi na kwa kufuata sheria na taratibu zilizopo, akibainisha kuwa Serikali haina dhamira ya kuwaonea wananchi bali kuhakikisha miradi ya umma inatekelezwa sambamba na kulinda haki za wananchi.
Aidha, Mhe. Dendego aliwaondoa hofu wananchi ambao nyumba zao zimewekewa alama ya “X”, akieleza kuwa alama hiyo haimaanishi kubomolewa kwa nyumba husika bali ni ishara ya kuwa nyumba hizo zimepitiwa katika hatua ya awali ya uhakiki, huku kamati maalum ikiendelea na tathmini ya kina kwa kuwafuata wananchi katika makazi yao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Mhe. Dkt. Vincent Mashinji, amesema Wilaya ya Manyoni ni salama na imejengwa katika misingi ya kusikilizana hata panapokuwepo mitazamo tofauti, bila migogoro kugeuka kuwa fujo. Amesema mgogoro huo uliwahi kufikishwa katika ofisi yake na kamati iliundwa, ambayo ilibaini kuwa zaidi ya wananchi 400 wanahusishwa na migogoro ya ardhi katika maeneo ya miradi ya umma ya maendeleo ikiwemo viwanda, shule, huduma za afya na VETA.
Dkt. Mashinji ameongeza kuwa Wilaya imefanya juhudi kubwa katika kushughulikia suala hilo, hatua iliyosababisha kumualika Mkuu wa Mkoa kuja kusaidia kusuluhisha changamoto hiyo kwa kiwango cha juu zaidi, akisisitiza kuwa kila mwananchi atapata haki yake kwa mujibu wa sheria na taratibu.
Katika mkutano huo, wananchi wameeleza furaha na matumaini makubwa baada ya kusikia kauli ya Mkuu wa Mkoa aliyewahakikishia kuwa ndani ya siku 14 mgogoro huo utakuwa umesuluhishwa, wakisema ahadi hiyo imewajengea imani mpya na kuwapa nafuu ya moyo kwamba changamoto yao ya muda mrefu sasa inaelekea kufikia tamati, huku wakiahidi kushirikiana na Serikali hadi suluhu ya kudumu ipatikane.
Kwa mujibu wa taarifa za Wilaya ya Manyoni, mgogoro wa ardhi katika maeneo ya miradi ya umma umedumu kwa muda mrefu kutokana na kukosekana kwa uhakiki wa kina wa umiliki wa ardhi kabla ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hali iliyosababisha sintofahamu kati ya wananchi na Serikali, na hivyo kuilazimu Serikali ya Mkoa kuingilia kati ili kuhakikisha haki za wananchi zinalindwa sambamba na utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya maendeleo.







SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.