Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, ameongoza timu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kufanya ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi leo tarehe 26 Januari 2026, kwa lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya elimu na afya na kuhakikisha matumizi sahihi ya fedha za umma.

Katika ziara hiyo, Dkt. Mganga alikagua miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Zahanati ya Kitongoji cha Mlongoji, unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na wananchi. Serikali Kuu imetoa Tsh 50,000,000 kwa ajili ya umaliziaji wa zahanati hiyo, huku wananchi wakichangia Tsh 2,614,000, wadau Tsh 2,750,000 na nguvu kazi yenye thamani ya Tsh 1,250,000. Aidha, Mfuko wa Jimbo ulitoa Tsh 10,000,000. Hadi sasa, jumla ya Tsh 13,437,815.51 tayari imetumika.

Ziara hiyo pia ilihusisha ukaguzi wa miradi ya elimu ikiwemo ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa katika Shule ya Msingi Kitaraka unaofadhiliwa kupitia Programu ya BOOST kwa gharama ya Tsh 92,000,000, ambapo hadi sasa Tsh 69,055,299 tayari zimetumika. Mradi huo unatarajiwa kunufaisha wanafunzi 667. Katika Shule ya Msingi Kazikazi, kamati ilikagua ujenzi wa madarasa ya awali na msingi pamoja na matundu ya vyoo, mradi unaogharimu Tsh 120,000,000 kupitia Programu ya BOOST.

Ukaguzi huo ulihitimishwa katika mradi wa ujenzi wa Shule mpya ya Msingi ya Kijobolo iliyopo Kitongoji cha Milumbi, unaotekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali na wananchi. Mradi huo umefadhiliwa na michango ya wananchi, Mfuko wa Jimbo, Halmashauri ya Wilaya ya Itigi na Programu ya BOOST kwa jumla ya zaidi ya Tsh 300,000,000, ambapo hadi sasa zaidi ya Tsh 214,000,000 tayari zimetumika.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt. Fatuma Mganga aliwataka wazazi na viongozi wa maeneo husika kuhakikisha watoto wote wanapata haki yao ya msingi ya elimu na kushiriki kikamilifu katika programu za lishe shuleni. Alisisitiza umuhimu wa ufuatiliaji wa karibu wa miradi ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati, kwa viwango vinavyokubalika na kwa kuzingatia thamani ya fedha.

Ziara hiyo ni sehemu ya mkakati wa Mkoa wa Singida wa kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi.




SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.