Serikali ya Mkoa wa Singida imeunda kamati ya kuchunguza na kufanya tathimini tukio la kuungua moto soko kuu la mjini Singida ili wafanyabishara waliopata janga hilo iangalie namna ya kuwasaidia.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe.Halima Dendego, akizungumza na wananchi na wafanyabishara leo baada ya kutembelea kukagua eneo la tukio, amesema kamati hiyo ifanya kazi hiyo kwa muda wa siku saba kuanzia leo.
Amesema kamati aliyoiunda itawajumuisha wafanyakazi wa serikali, Kamati ya Usalama ya Mkoa na mameneja wa benki zote zilizopo mkoani hapa na kwamba baada ya tathimini hiyo kazi ya kurejesha miundombinu ya soko hilo itaanza mara moja.
“Ndani ya kamati hizi kutakuwa na wataalam wa fedha,wataalamu wa biashara na wataalam wa afya pia kwani wenzetu wamepata mshtuko lazima tuwajue mmoja mmoja wapo wapi ili warejee katika hali salama na kazi hiyo inaanza leo na tumewapa siku saba wamalize kazi hiyo na sisi tutaanza kusafisha eneo hilo kwa ajili ya kujenga kwa haraka,” amesema.
“Naomba nitoe salamu za pole kutoka kwa Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan, tulimpa taarifa za awali na amenituma tukae mimi na kamati yangu kuweka kambi hapa ili tumjulishe uharibifu uliotokea hapa, lakini pia Waziri wa Tamisemi, Mhe.Mohamed Mchengerwa anawapa pole,” alisema Dendego.
Aidha,Dendego amekipongeza Kiwanda cha Pamba cha Biousastain na kiwanda cha Meru ambavyo vimeweza kusaidia kutoa vitendea kazi katika kufanikisha kazi ya kuzima moto.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Martha Mlata, amewapa pole wafanyabiashara kwa janga hilo na kuwaahidi kwamba ana imani kubwa kuwa Serikali itarejesha miundombinu ya soko hilo ili shughuli za biashara ziendelee kama kawaida.
Kadhalika,Mlata amelipongeza Jeshi la Zimamoto na Ukoaji, Jeshi la Polisi na wananchi kwa jinsi walivyoweza kushirikia katika zoezi la uokoaji ambapo hakukuweza kutokea tukio la kupora mali za waathirika.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Singida, Godwin Gondwe, alisema ulinzi utaendelea kuimarishwa katika soko hilo ili uporaji woowote usiweze kufanyika.
Mwenyekiti wa Soko Kuu la Singida, Hassan Mboroo, alisema moto katika soko hilo ulianza kuwaka saa 3:40 usiku wa kuamkia leo katika duka la kuuza vifaa vya ujenzi baadaye kuenea katika maduka mengine.
Amesema zoezi la kuuzima lilianza kufanyika muda huo na kufanikiwa kuuzima hapo baadae ambapo jumla ya maduka 15 yameteketea kwa moto zikiwamo bidhaa zilizokuwemo na kusababisha hasara kubwa kwa wafanyabiashara.
Mboroo alisema kufuatia tukio hilo kuna haja kwa serikali kuliboresha soko hilo kwa kuweka katika mpangilio mzuri ili kunapotokea majanga kama haya ya moto magari ya kuzimia moto yaweze kupita kwa urahisi kufanya kazi ya uokozi.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.