Wito umetolewa kwa wananchi mkoani Singida kutumia fursa zitakazopatikana wakati wa Mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) utakao anza hivi karibuni mkoani hapo ili waweze kujiongezea kipato na kuondoa umaskini.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge ametoa wito huo hivi karibuni wakati akifungua mkutano uliofanyika katika ukumbi wa mikutano ofisi za Mkaguzi wa Hesabu na kuhusisha Wakuu wa Idara mbalimbali pamoja na wafanyabiashara wa Mkoa wa Singida na kuwataka kuzitumia fursa mbalimbali ambazo zitapatikana wakati wa ujenzi wa bomba hilo.
Amesema ujenzi wa bomba hilo utakuwa na jumla ya vituo 14 katika Wilaya na Mikoa mbalimbali ambapo kituo cha 11 kitakuwa mkoani Singida katika kijiji cha Ntondo kilichopo Manispaa ya Singida Mjini.
Dkt. Mahenge amesema kituo hicho kitakuwa na watumishi kuanzia 1,000 hadi 2,000 ambao watahitaji kula, kulala na kunywa hivyo wananchi wa Singida wanatakiwa kutumia fursa hiyo kwa kuanza kuwekeza kwa kujenga vyumba za kupangisha, nyumba za kulala wageni pamoja na ufugaji wa kuku ili wapate kipato na watoe ajira kwa wengine.
Aidha Serikali tayari imeandaa mazingira wezeshi yanayovutia uwekezaji kwa kutengeneza barabara na kuweka umeme ili wananchi waweze kuendelea na mapambano ya kuondoa umasikini alifafanua Mkuu wa Mkoa.
Akimalizia hotuba yake Mhe. RC ameeleza kwamba Serikali mkoani hapo imeendelea kuongea na mabenki mbalimbali wapunguze riba katika mikopo yao ili iweze kuwavutia wateja .
Katibu Tawala Mkoa wa Singida Bi Dorothy Mwaluko moja ya wadau katika mkutano huo wakati akimkaribisha Mkuu wa Mkoa amesema bomba hilo litakuwa na urefu wa kilometa 140 kwa Singida ambapo litapita katika wilaya tatu za Iramba, Mkalama na Singida Vijijini.
Katibu Tawa huyo amebainisha kwamba jumla ya vijiji 31 na kata 17 vitapitiwa na mradi huo hivyo kuwataka wananchi wa maeneo husika kuhakikisha wanatumia fursa kwa ajili ya maendeleo ya Mkoa wa Singida na taifa kwa ujumla .
Kwa upande wake Bw. Safiel Msovu kutoka Shirika la Maendeleo ya Petrol Tanzania (TPDC) katika wasilisho lake mbele ya mgeni rasmi amebainisha kwamba urefu wa Bomba kutoka Uganda hadi Tanzania ni km 1,443. Urefu upande wa Uganda ni km 296 na Tanzania ni km 1,147. Uwezo wa Bomba kusafirisha mafuta ni mapipa 216,000 kwa siku.
Aidha Bw. Msovu amefafanua kwamba mradi huo ni mkubwa na unagharimu kiasi cha dola bilioni 3.5 sawa na shilingi triloni nane (8) na unatarajiwa kuanza hivi karibuni kwa kuwa mikataba muhimu imekamilika.
“Wanahisa katika mradi huo ni kampuni ya ufaransa inayojulikana kwa jina la Total, Uganda kupitia shirika la mafuta la UNOC, kampuni ya kichina ya CNOOC na Shirika la Uendelezaji wa Petrol nchini (TPDC)” alisema Bwana Msovu.
Kwa mujibu wa muundo wa sasa wa mgawanyo wa hisa, kampuni ya Ufaransa Total itamiliki asilimia 62, kampuni ya China CNOOC asilimia 8, UNOC ya Uganda itamiliki asilimia 15 na asilimia 15 iliyobaki itamilikuwa na Tanzania kupitia kwa kampuni yake ya maendeleo ya mafuta TPDC.
Hata hivyo alimalizia kwamba mradi huo unategemewa kujengwa kwa kipindi cha miaka mine (4) na unategemewa kutoa huduma kwa miaka isiyopungua 25, alimalizia bwana Safiel Msovu
Wafanyabiashara mkonia Singida kwa umoja wao wamesema kwamba wamejipanga kutumia fursa hiyo ila wameomba Serikali kuendelea kutengeneza mazingira wezeshi ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusiana na maendeleao ya mradi huo
Mwisho.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.