Serikali kwa kushirikiana na Tanzania Agricultural Modernization Association (TAMA) na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) leo imetambulisha rasmi Mradi wa YEFFA ambapo ni mradi wenye lengo la kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika kilimo cha kisasa kupitia mafunzo ya ufundi stadi, ajira na ujasiriamali. Mradi huu, unatekelezwa na Tanzania Agricultural Modernization Association (TAMA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na kufadhiliwa na Shirika la AGRA.

Hayo yamejiri wakati wa kikao maalum cha kuutambulisha mradi huo kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Januari 27,2026 na kuwashirikisha wadau mbali mbali wakiwemo Viongozi wa Dini,Maafisa Mipango, wadau wa elimu na wengineo kwa lengo la Kwenda kuwa mabalozi wa kuutambulisha mradi huo kwa jamii.

Akizungumza wakati akitoa wasilisho katika kikao hicho, Bw. Frank Shinge ambaye ni Afisa Ufuatiliaji na Tathmini mradi wa YEFFA ,amesema kuwa mradi huo unalenga kuwajengea uwezo vijana kupitia mafunzo ya ufundi stadi katika uendeshaji na matengenezo ya mitambo ya kilimo, mifumo ya umwagiliaji pamoja na usindikaji wa mazao.
“ Mradi huu unatekelezwa katika mikoa ya Singida, Tabora, Dodoma na Manyara, na unafadhiliwa na Shirika la AGRA huku Utekelezaji wake ulianza mwezi Novemba 2025 na unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba 2027.’’
Kupitia mradi huu, jumla ya vijana 1,525 watanufaika moja kwa moja na mafunzo ya kiufundi, ambapo asilimia 70 wanatarajiwa kuwa wanawake, huku vijana 130 wenye mahitaji maalumu wakijumuishwa kikamilifu katika mpango huu. Kupitia vijana hawa, zaidi ya wakulima wadogo 32,500 watanufaika kwa kupata huduma za mitambo ya kilimo, hali itakayoongeza uzalishaji, ufanisi na ubora wa shughuli za kilimo.

Bw.Frank alisema kuwa YEFFA ni chachu ya mabadiliko katika sekta ya kilimo kwa kuwa itawapa vijana ujuzi wa vitendo unaohitajika katika soko la ajira na kuwawezesha kujiajiri au kuajiriwa. Aliongeza kuwa mradi huu unakuja wakati muafaka wa kuimarisha kilimo cha kisasa na chenye tija katika mkoa wa Singida na maeneo ya jirani.
Kadhalika Katika kuhakikisha mradi unakuwa jumuishi na unaowafikia vijana wote, waandaaji wa YEFFA wamesema kuwa wamejipanga vizuri zaidi kuwapokea vijana wenye mahitaji maalumu kwa kuwaandalia mazingira rafiki ya ujifunzaji. Ambapo wameweka mikakati ya kuhakikisha upatikanaji wa nukta nundu kwa wasioona, njia zinazopitika kwa walemavu wa viungo pamoja na matumizi ya lugha ya alama kwa wanafunzi wasiosikia na wasioweza kuzungumza, ili kila kijana apate fursa sawa ya kushiriki kikamilifu katika mafunzo.
Akizungumzia katika suala la utekelezaji, Bw.Bura chepa Mratibu wa Mradi wa YEFFA kwa upande wa VETA,amesema kuwa VETA itakuwa na jukumu la kutoa mafunzo ya kiufundi kwa vijana, huku TAMA ikisimamia uratibu wa mradi, ufuatiliaji na tathmini pamoja na kuwaunganisha wahitimu na fursa za ajira na ujasiriamali katika sekta ya kilimo cha kisasa.
Mradi wa YEFFA pia unatarajiwa kusaidia kuanzishwa kwa biashara 600 zinazoendeshwa na vijana, kutoa fursa 600 za mafunzo ya vitendo pamoja na kuwezesha takribani vijana 6,500 kupata ajira au kujiajiri kupitia mbinu ya mafunzo ya wawezeshaji kwa wenzao. Kupitia jitihada hizi, YEFFA unatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo ya kilimo chenye tija, ushindani na ujumuishi nchini Tanzania.

Mgeni rasmi wa hafla hiyo,Bw.Somboi Harold ambaye ni Afisa Kilimo wa Mkoa wa Singida Amezungumza wakati wa kufunga kikao akiwasisitiza washiriki wa kikao hicho kuhakikisha wanakwenda kuwa mabalozi wazuri kwa jamii katika kuhakikisha wanapeleka taarifa hizi njema kwa walengwa ili waweze kunufaika na fursa hiyo ambayo itakwenda kuwa chachu ya maendeleo kwa vijana,wanawake na watu wenye mahitaji maalumu kwa kupata mafunzo bora.

Alisisitiza kuwa mradi huo ni hatua muhimu katika kubadili taswira ya kilimo kwa vijana na kuongeza ajira katika Ukanda wa Kati wa Tanzania.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.