Serikali, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo imedhamiria kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa vijana kwa kuimarisha miundombinu msingi ya Chuo cha Uhasibu nchini-TIA, Tawi la Singida kwa gharama ya Sh. Bilioni 13.5/-.
Jitihada hizi zinajidhihirisha kupitia mradi wa ujenzi wa jengo la ghorofa tano katika Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA), Tawi la Singida linalojengwa na Serikali kupitia Wizara ya fedha, kwa kumtumia mkandarasi mzalendo.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya mradi huo iliyofanyika Octoba 18, 2024 katika Chuo cha Uhasibu Singida, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego amesema mradi huo unaogharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 13.5, utaboresha mazingira ya chuo hicho muhimu kwa fani ya uhasibu nchini.
Mkuu wa mkoa wa Singida, Halima Dendego amesema makabidhiano hayo chini ya Serikali, ni kati ya uongozi wa TIA na Kampuni ya SALEM CONSTRUCTION LTD, inayojenga mradi huo.
Amefafanua kuwa, ujenzi wa ghorofa hilo ni moja ya jitihada za Serikali ya awamu ya sita kuhakikisha chuo hicho kinapanuka zaidi ili kuogeza upatikanaji wa elimu ya juu pamoja na kupendezesha pia mji wa Singida unaostawi kwa kasi kutokana na ujirani wake na makao makuu ya nchi (Dodoma).
Dendego amesema kuwa, pia ujenzi wa miundombinu ya barabara kwa kiwango cha lami, zinazounganisha mkoa wa Singida na mikoa mingine nchini, inachochea ukuaji wa mji wa Singida.
"Nimefurahi, na tumefurahi mno, na tumefarijika mno, kwamba tayari safari yetu ya maendeleo tumeshikwa mkono na sisi tunamwambia Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwamba hatutamwangusha...tutatumia fursa zinazotoka Serikalini, lakini nitajaribu kuunganisha wadau wengine na Serikali kuhakikisha Singida inakua, tunamwomba Mwenyezi Mungu atupe uhai, tunamwomba Mwenyezi Mungu atupe afya,"amesema Dendego.
Aidha Dendego ameipongeza Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) kwa kumpatia mkandarasi mzawa (SALEM CONSTRACTION LTD) mradi huo, hali inayoonyesha imani kubwa kwa makampuni ya kizalendo, kwamba yakipewa nafasi, yanayaweza kufanya kazi kubwa na nzuri, iliyotukuka kwa maslahi ya Taifa.
"Kwa hiyo hii ni kazi kama kazi nyingine yoyote, ya utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi...kwa hiyo mimi mama yako napenda vitu vizuri, wanajua wale ninaowaongoza, naomba sana mradi huu uwe na ubora, na ukamilike kwa wakati na thamani ya fedha iweze kuonekana," amesisitiza Dendego.
Kadhalika Dendego amemtaka mhandisi mshauri, Kampuni inayomsimamia mkandarasi huyo, kuhakikisha anatumia muda wake mwingi akiwa eneo la mradi, vinginevyo atawajibika kwa lolote litakalochangia mradi kujengwa chini ya kiwango.
"Rai yangu kwa Mkandarasi Mshauri, kuanzia tunapobomoa majengo ya zamani mpaka tunakamilisha hili jingo jipya, macho yako na masikio yako yawe hapa...sitapenda kuona wala kusikia kuna siku mnaniita niwapatanishe kati yako wewe na mkandarasi hilo wala sitaki kulisikia kwa hiyo kaeni muelewane mfanye kazi nzuri," alisisitiza Dendego.
Ili kuonyesha amedhamiria mradi huo kujengwa kwa kiwango na kukamilika kwa wakati, RC. Dendego aliwahakikishia kwamba atafanya kila njia ili jiwe la msingi la mradi huo lije kuwekwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan.
Mradi huo unatekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya fedha, Wizara ya elimu Sayansi na Teknolojia, chini ya benki ya Dunia, inayotekeleza mradi huo wa mageuzi ya kiuchumi na utekelezaji wa mradi huo ulianza Septemba 2021 na taasisi mbalimbali za elimu zipatazo 22 nchini zilipatiwa fedha kwa ajili ya mradi huo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego (kulia) akimkabidhi Mkandarasi wa Kampuni ya Salem Contruction LTD, cheti cha makabidhiano ya Mradi wakati wa hafla iliyofanyika katika ukumbi wa chuo cha Uhasibu Singida.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.