RC Singida Dkt. Binilith Mahenge amefanya ziara ya kikazi kwenye kituo cha ukaguzi wa pamoja wa magari (one stop centre ) kinacho milikiwa na Wakala wa Barabara TANROAD kilichopo Kijiji cha Mhalala wilayani Manyoni mkoani hapa ambacho kimelenga kupunguza muda na gharama ya usafirishaji wa mizigo kupitia Barabara ya ukanda wa Kati.
Akiongea baada ya ziara hiyo Dkt. Mahenge amesema Kituo hicho cha ukaguzi ni muhimu katika kukuza uchumi wa Mkoa na kutoa ajira kwa wananchi wengi endapo kitakamilika hivyo kuwataka wataalamu kuanza kufikiria namna ya kumalizika Mradi huo.
Aidha Mahenge ametoa maelekezo kwa Meneja wa TANROAD kuharakishwa kwa mchakato wa kumalizika kwa majadiliano baina yao na Mkandandarasi ili fedha za wafadhili ziendelee kukamilisha kazi hiyo.
Amesema Serikali haiwezi kuacha Kituo hicho kikapotea wakati kimetumia fedha nyingi na bàadhi ya wananchi wameshaanza Kuwekeza ili kuweza kufanya Biashara endapo kituo hicho kitakamilika.
Aidha Dkt.Mahenge amesema atashirikiana na Mawaziri wa Wizara husika katika kupambana na umaliziaji wa Mradi huo ambao ulianza toka Machi 2017 ambapo mpaka sasa umefikia asilimia 60.
Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa Mhandisi Heldaus Jerome Msimamizi wa mradi huo amesema kwa sasa magari ya mizigo husimama katika vituo 31 katika Barabara ya Kanda ya Kati ambapo ucheleweshaji umekuwa ni mkubwa na tija imekuwa ni ndogo ikilinganishwa na matumizi ya Kituo hicho cha pamoja.
Amesema kati ya vituo hivyo 31 vinavyotumika 8 ni vituo vya mizani 20 ni vya ukaguzi wa Polisi vitatu ni ukaguzi wa mapato ambavyo viko Kati ya Dar es salaam hadi Rwanda na Burundi na DRC vyenye umbali wa kilometa 1000.
Amesema Mradi huo umefikia asilimia 60 ambapo kazi zilizobaki kwa sasa ni Ujenzi wa tabaka la mhimili wa juu la zege na la Kati ikiwa ni pamoja na Barabara zinazokwenda katika nyumba za makazi ya watumishi.
Aidha Mhandisi Jerome amesema Mradi huo umegharimu kiasi cha sh.Bilion 9.6 ikiwa ni manunuzi ya vifaa pamoja na malipo ya makandarasi.
Kwa upande wake Mhandisi Matare Masige Meneja wa TANROAD Mkoa wa Singida amesema Mradi huo ulikuwa ukitekelezwa na Mkandarasi Impress di construction Mhandisi Mantovan kutoka Italia amabaye alisitisha mkataba wake na TANROAD baada ya kuona kama Serikali inamcheleweshea urejeshaji wa Kodi zake alizozilipa kinyume na mkataba wa kazi.
Amesema mkataba wa Mkandarasi huyo ulikuwa na msamaha wa Kodi katika ununuzi wa vifaa jambo ambalo Serikali ilitaka kuhakiki kama manunuzi ya vifaa hivyo yalifanyika na kama vifaa hivyo vilifika katika maeneo yaliyokusudiwa jambo ambalo lilionekana kuchelewa.
Mhandisi Matare akabainisha kwamba Makandarasi amelipwa Bilioni 9.6 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na malipo ya awali wakati Mhandisi Msimamizi akiwa amelipwa jumla ya Sh.Milioni 651.2 alisisitiza.
Hata hivyo Mhandisi Matare akauomba uongozi wa Wilaya na Mkoa kusaidia kuzuia uvamizi wa eneo la Mradi huo unaofanywa na bàadhi ya wananchi hao ambao tayari walishalipwa fidia ya eneo hilo.
Akijibu hoja hiyo RC Mahenge akawaangiza wakala hao wa Barabara kuweka bikoni ndefu pamoja na matangazo kama hatua ya kupambana na uvamizi wa maeneo hayo.
Juma Kilimba Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida akawataka Wabunge wa mkoa huo kujitahidi kuongeza uelewa juu ya Mradi huo ili wasaidie kuharakishwa ukamilishwaji wa mazungumzo baina ya pande mbili hizo.
Akawataka TANROAD kuendelea kulinda rasilimali zilizopo eneo hilo la Mradi ili pasitokee uharibifu wa namna yoyote kwa kuwa Serikali itaendeleza Mradi huo.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.