Mamlaka ya Maji Safi na Mazingira Mkoani Singida (SUWASA) wametakiwa kutumia mbinu mbadala kuongeza ukusanyaji wa mapato ili waweze kuendeleza miundombinu na kupunguza upotevu wa maji.
Akiongea leo tarehe 07.09.2021 katika ukumbi wa mikutano SUWASA mara baada ya kutembelea miradi mbalimbali ya maji iliyojengwa na mamlaka hiyo RC Singida Dkt. Binilith Mahenge amesema ukusanyaji wa mapato ukisimamiwa vizuri utasaidia kuongeza mapato na kukarabati miundombinu na usambazaji wa maji katika maeneo mengi Zaidi kwa kutumia fedha za ndani.
Aidha Dkt. Mahenge amebainisha kwamba kiasi cha maji yanayopotea kwa Mkoa wa Singida ni asilimia 33.4 ambayo ni kiasi kikubwa kikilinganishwa na asilimia 22 ya upotevu inayokubalika hivyo kuwataka SUWASA kuhakikisha upotevu unapungua.
Hata hivyo Dkt. Mahenge ameipongeza SUWASA kwa kuanzisha miradi mingi ya maji ambayo imejengwa kwa kutumia fedha za ndani na kwa viwango vinavyokubalika.
RC ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha zaidi ya shilingi bilioni 3.07 ili kutekeleza miradi ya maji iliyopo Manispaa ya Singida, Wilaya ya Iramba na Ikungi
Nawapongeza sana kwa kazi nzuri mliyofanya, Miradi mingi iliyojengwa ina viwango vinavyokubalika kwa fedha za ndani hii inaonesha ubunifu mkubwa mliutumia katika kutekeleza miradi hii, niwaombe muendelee kusimamia vizuri makusanyo ili muweze kuanzisha miradi mingine. Alisema Dkt. Mahenge
Aidha ametoa wito kwa wananchi wote mkoani hapo wanaotumia huduma ya maji kuhakikisha wanalipia huduma hiyo kwa wakati ili kusaidia Mamlaka kuendelea kusambaza huduma kwa watu wengine .
Naomba muandae orodha ya Taasisi na watu wote wanao daiwa nizipate ofsini kwangu, lazima mtu aliyepatiwa huduma ya maji na akayatumia alipe, nitoe wito kwa yeyote anayejua kwamba ana deni la maji alipe kabla orodha hiyo haijanifikia. Alisisitiza RC Mahenge.
RC amewakumbusha watumishi wa SUWASA kuhakikisha kwamba hakuna udanganyifu unaofanyika katika usomaji wa mita na kuacha ukadiriaji kwa mteja.
Akimalizia hotuba yake Dkt. Mahenge amewaagiza watumishi kufanya ukaguzi wa kawaida utakaobaini ubora wa maji katika visima binafsi vinatoa huduma kwa wananchi na kuyapima ili kulinda afya za watu.
Awali Mkurungenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji safi na mazingira Mkoani Singida (SUWASA) Mhandisi Patrick Nzimba amesema mkoani hapo wametekeleza jumla ya miradi ya maji saba (7) inayogharimu kiasi cha shilingi bilioni 3.075 katika Kata za Unyambwe, Minga, Mungumaji na Vijiji vya Misigiri na Ulemo
Aidha amebinisha kwamba Mamlaka ina mpango wa kuongeza uzalishaji wa maji kwa kuchimba visima 11 kupitia fedha za miradi 28 ya maji lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wengi wanapata maji.
Mhandisi Patrick amefafanua kwamba SUWASA kwa kushirikiana na RUWASA watakarabati miradi nane (8) pembezoni mwa mji katika maeneo ya Unyamikumbi A, Mtamaa B, Manga, Ititi, Uhamaka,Unyianga Mtamaa A na Mwankoko A ambayo kwa sasa haitoi huduma ya maji.
Ameendelea kusema kwamba wameweka mkakati wa kuhakikisha wanaongeza mtandao wa maji kwa kusambaza mabomba yenye urefu wa zaidi ya Kilometa 10 katika maeno ambayo hayana huduma hiyo.
Hata hivyo ameongeza kwamba changamoto kubwa katika utoaji wa huduma ya maji ni uhaba wa mitandao ya majitaka ambayo huathiri mazingira na tayari mipango ya uanzishwaji wa mradi huo umekamilika.
Changamoto nyingine ni kupungua kwa uwezo wa visima kuzalisha maji na vingine kuwa na maji chumvi pamoja na uwepo wa mtandao wa mabomba ya zamani wenye urefu wa kilometa 40 ambayo husababisha upotevu wa maji. Alisema Mhandisi Patrick.
Aidha Mhandisi Patrick amemueleza RC kwamba baadhi ya wateja wamekuwa kikwazo kwa kuwa hawalipi madeni yao kulingana na huduma ya maji wanayoipata hivyo kusababisha deni la shilingi milioni 581.32 ambapo taasisi za Serikali pekee zinadaiwa kiasi cha shilingi milioni 305.
mwisho
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.