Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Singida imekifungia chuo kilichopo chini ya Masjid Shafii katika eneo la Mwaja Manispaa ya Singida kutokana na Shughuli zake kutofahamika, kukosa usajili na miundombinu yake kutoridisha.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulizi na Usalama ya Mkoa ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amekifungia chuo hicho leo asubuhi kutokana na kutokuwa na usajili na hivyo kutumia usajili wa msikiti namba 4834 pia kujiendesha bila ya kuwa na mtaala wowote unaoonyesha mafunzo yanayotolewa na hatma ya wanaosoma hapo.
Akiwa ameambatana na Wajumbe wote wa Kamati hiyo Dkt Nchimbi amesema baada ya kukifunga, wahusika wafuatilie usajili wa chuo hicho na kuhakikisha wanafunzi 80 ambao wametoka ndani na nje ya Mkoa wa Singida wanarudi makwao mara moja.
Ameongeza kuwa waalimu wawili wa chuoni hapo ambao ni raia wa kigeni kutoka Marekani na Yemen warudi katika makao makuu ya taasisi yao kwakuwa walikuja Singida kwa ajili ya chuo na sasa kimefungwa, huku akimuagiza Afisa Uhamiaji wa Mkoa kutoa usaidizi ili raia hao wafike salama wanakostahili kwenda.
“Chuo hiki kifungwe mara moja, fuatilieni usajili kwanza kwakuwa sheria za nchi zinataka chuo chochote kile lazima kiwe na usajili, pia wanafunzi wote warudi makwao, Kamanda wa Polisi Mkoa hakikisha unasimamia watoto hawa wanafika makwao salama”, ameagiza Dkt. Nchimbi.
Amesema pamoja na chuo hicho kutokuwa na usajili, bado wana changamoto nyingine ambazo wanatakiwa kuzishughulikia kabla hawajafuguliwa ikiwemo miundombinu ya mabweni na vyoo vya kujitosheleza.
“Tungependa kujua aina ya mafunzo mnayotoa na yatamuwezesha vipi atakayehitimu kujikimu kimaisha pamoja na kuchangia maendeleo ya taifa, pia Afisa Afya amekagua na kuona mapungufu, hakikisheni mnakuwa na vyoo pamoja na mabweni ya kutosha, mtakapokuwa tayari hata kama ni ndani ya wiki moja au mwezi hata mwaka ndipo nitakifungua tena chuo hiki”, amesisitiza.
Dkt Nchimbi ameongeza kuwa Serikali inapenda na kuthamini taasisi za kidini kwakuwa zinatoa malezi ya kimaadili ya kuwajenga wananchi kuwa waadilifu na wachapakazi hivyo wanachotakiwa kufanya ni kufuata taratibu na sheria katika kuanzisha chuo chao.
Amesema nia yake ni kuona chuo hicho kinakamilisha taratibu za kisheria ndipo kifunguliwe huku akiamini kuwa kitaweza kuwa chuo bora na cha mfano wa kuigwa kwa kuzalisha wana taaluma waadilifu na wachapa kazi huku akisisitiza kuwa Msikiti wa Masjid Shufaa haujafungwa, uko halali hivyo waumini wake waendelee kuswali.
Imam wa Msikiti huo Mohamed Said ambaye amekubaliana na uamuzi wa Mkuu wa Mkoa Dkt Nchimbi amesema chuo hicho kinakabiliwa pia na changamoto ya kukosa umeme, maji na Chakula.
Said amesema anaishukuru kamati ya ulinzi na usalama kwa ushirikiano wanaopewa hadi kufikia hapo walipo na kusisitiza kuwa ushirikiano huo umeletwa na uongozi mzuri wa Mkoa wa Singida.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.