Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba amewataka Wakulima Mkoani Singida kuendelee kuandaa mashamba kwa ajili ya kilimo wakati Serikali ikiendelea na mchakato wa kuleta mbolea ya kutosha katika Wilaya mbalimbali.
Kauli hiyo ameitoa leo katika Kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi hiyo ambacho kiliwakutanisha Wakuu wa Wilaya, Wakurungenzi na Maafisa kilimo wa Halmashauri zote Mkoani lengo likiwa ni kujadili changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa mbolea, Maandalizi ya mashamba darasa na mashamba darasa pamoja na changamoto za wadaiwa.
RC Serukamba amewataka wakulima kuendelea na maandalizi ya msimu wa kilimo kwa kuwa swala la upatikanaji wa mbolea linashughulikiwa na viongozi wa Serikali kuhakikisha mbolea inamfikia kila mkulima huku akiwataka Wakuu wa Wilaya kuendelea kuwakumbusha wahusika mara kwa mara.
Awali akichangia mada juu ya hali ya upatikanaji wa mbolea Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskasi Muragili amesema Wakulima wa Wilaya yake wana uhitaji mkubwa wa mbolea kwa ajili ya Kilimo hivyo zifanyike juhudi mbalimbali kuhakikisha Mawakala wanaleta mbolea ya kutosha kwa wakati.
Aidha Muragili ameeleza kwamba uwezo wa Mawakala kununua kiasi kikubwa cha mbolea ni mdogo jambo ambalo limesababisha hofu kwa Wakulima kukosa mbolea wakati msimu ukiwa umekaribia.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro, ameeleza kwamba Wilaya hiyo mpaka sasa hakuna mbolea iliyoingia jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa na Wakulima.
Jerry ameeleza kwamba Wakulima Wilayani hapo walishakamilisha maandalizi ya msimu wa kilimo kwa kupata mbegu na kusafisha mashamba jambo lililobaki ni kuwa na uhakika wa mbolea tu alieleza.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleimani Mwenda, akizungumza wakati wa kikao hicho.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleimani Mwenda, amesema wao wameweza kupata mbolea kwa kiasi kikubwa kwa sababu wakulima walikuwa tayari wameshachanga fedha hivyo kuwafanya wa mawakala wa mbolea kupata kushawishika zaidi.
Amesema kununua Mawakala wengi hawana mtaji mkubwa hivyo wakihakikishiwa fedha wanaweza kuleta eneo lolote ili waweze kupata fedha na kuagiza mzigo mwingine.
Akihitimisha mjadala huo Mkuu wa Mkoa amesema Serikali ipo makini katika zoezi la usambazaji wa mbolea ili kuepusha uvushaji wa mbolea hiyo kwenda nje ya nchi kwa kuwa imeweka fedha nyingi za ruzuku.
Mwisho
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.