Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, amewataka viongozi na wadau wote wa kilimo mkoani hapa kuweka mikakati thabiti ya kuwaelimisha wakulima ili waweze kuingia na kuchochea mpango wa kilimo hai kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao maradufu.
Dk. Mganga amesema hayo wakati akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, katika ufunguzi wa mkutano wa wadau wa kilimo (Multi-Stakeholder Dialogue) uliofanyika mjini Singida.
Mkutano huo ulihusisha viongozi wa serikali, sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), na wakulima, ambapo wadau walijadiliana juu ya fursa na changamoto za kilimo endelevu, kwa kuzingatia nguzo tatu kuu: watu (people), mazingira (nature), na uchumi (economy).
Akizungumza kwenye kikao hicho, Dkt. Mganga amesema Mkoa wa Singida ni miongoni mwa wazalishaji wakuu wa mazao ya biashara na chakula nchini, ikiwemo alizeti, pamba, karanga na mahindi, hivyo iwapo mikakati thabiti itawekwa ya kuwaingiza wakulima katika mpango wa kilimo hai, kutaongeza uzalishaji na kulinda mazingira ya mkoa huo.
Kwa upande wao, wakulima walioshiriki mkutano huo walieleza furaha yao kushirikishwa moja kwa moja katika majadiliano, jambo walilosema linaongeza uelewa na nafasi yao kushiriki katika mchakato wa kutengeneza sera za kilimo ngazi ya mkoa.
“Leo nimefurahishwa sana kuona sisi wakulima wa Singida tumewekwa pamoja na serikali, sekta binafsi na mashirika kama HELVETAS Tanzania. Kupitia mazungumzo haya tumejifunza njia za kulima kijani zinazolinda ardhi na maji, huku pia zikiongeza kipato chetu. HELVETAS na wadau wengine wametufundisha mbinu bora, wametupa mbegu na hata kutuunganisha na masoko. Mimi binafsi nimeona mavuno yangu yakiongezeka na ninaamini Singida inaweza kuwa kiongozi wa kilimo hai Tanzania.”
Mashirika yaliyojitokeza kushirikiana na serikali na wakulima katika kikao hicho ni pamoja na Regenerative Production Landscape Collaborative (RPLC), Laudes Foundation, GIZ na HELVETAS Tanzania, ambapo wote walionesha dhamira ya kusaidia wakulima kupitia elimu, teknolojia, na sera shirikishi zinazochochea kilimo cha kijani.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.