Halmashauri za Wilaya zimetakiwa kuimarisha vyanzo vya mapato na mifumo ya ukusanyaji fedha ikiwa ni pamoja na kubuni miradi mipya itakayoongeza mapato ya Serikali.
Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa alipokutana na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
Amesema wapo watumishi na mawakala ambao wamepewa kazi ya ukusanyaji wa mapato lakini hawapeleki fedha Benki na wengine kuzitumia kwa matumizi yao binafsi hivyo kuwataka viongozi kuwachukulia hatua wote waliosababisha upotevu wa fedha hizo.
"Mnaweka mawakala kwenye ukusanyaji wa mapato ambao hamna mikataba nao, niwaombe Madiwani itisheni hiyo mikataba muikague na wachukulieni hatua watumishi ambao wamekula Milioni 300" alisema.
Hata hivyo ametoa onyo kwa Maafisa Tehama ambao wanaingilia mifumo ya ukusanyaji wa fedha ili kukwepesha fedha kutosomeka kwenye mifumo hivyo na kusababisha upotevu wa fedha kupitia mashine za Posi.
Kwa upande wake Naibu Waziri ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa Dr. Festo John Dugange amesema TAMISEMI ni Wizara ya wananchi hivyo watumishi wakisimamia taratibu zinazotakiwa Serikali itakuwa imefanikiwa kwa zaidi ya asilimia 70.
Dr. amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba Tamisemi wamepokea hizo changamoto na watazifanyia kazi ili kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma kama ilivyokusudiwa.
Aidha amewataka watumishi kuachana na vitendo vya kinyume na maadili kwa sababu kwa yeyote atakayehujumu au kufanya jambo kinyume atakamatwa kwa kuwa Serikali ni kama hewa inapatika popote alisisitiza Naibu Waziri.
Hata hivyo Naibu Waziri amekiri kuwepo kwa changamoto katika ukusanyaji wa mapato ya ndani jambo ambalo amesema wamelipokea na wanaendelea kulifanyia kazi ili kurekebisha hali hiyo.
Mwisho
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.