Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Daktari Fatuma Mganga Mei 8,2025 ameongoza timu ya ufuatiliaji na utekelezaji wa miradi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Halmashauri ya wilaya ya Ikungi akiongozana na wataalamu mbalimbali kutoka katika ngazi ya Mkoa na Halmashauri.
Awali walifanya Ukaguzi katika eneo la miradi wa ujenzi wa vyumba vya duka 21,mgahawa na vyoo vya matundu saba na bafu mbili lenye makadirio ya shilingi 285,000,000 inayojengwa kwa mkataba na Jeshi la Magereza Mkoa wa Singida.
Akisoma taarifa hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Bw.Edward Millinga amesema kuwa Mradi huo unatarajiwa kuwa na faida mbalimbali kwa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi na wananchi kwa ujumla kwa kuongeza eneo la upatikanaji wa huduma mbalimbali za mahitaji huku Halmashauri kuongeza mapato kutokana na kodi inayotarajiwa kuwa Tsh Milioni themanini kwa mwezi.
Kadhalika timu hiyo ilitembelea miradi wa ujenzi wa vyumba 20 vya maduka ya biashara katika eneo la stendi mpya ya Ikungi unaojengwa kwa hisani (miradi ya uwajibikaji)ya Kampuni ya Uchimbaji madini ya SHANTA ambapo asilimia 40 ya bajeti inatumika kutekeleza vipaumbele vya miradi inayozunguka mgodi huo.
Niceforus Mgaya,Mkuu wa Divisheni ya Mipango na Uratibu amesema kuwa Mradi huo ulioibuliwa na Halmashauri ya Wilaya ambapo asilimia 60 ya bajeti yake ilitengwa mwaka 2024 ukiwa na thamani ya shilingi 172,500.
Mhandisi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Eng.Lidya Mfalila alishauri kuhusu umaliziaji bora wa majengo hayo (finishing)kwa kuhakikisha kuwa inamalizika kwa ubora wa hali ya juu huku wakizingatia ujengaji bora wa vyoo kwa kuhakikisha wanatumia tamani iliyo sahihi kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza endapo hakitajengwa katika misingi sahihi hususani katika maeneo hayo ya uuzaji wa vyakula.
Kadhalika walifanya ukaguzi katika njia za kutembelea (Walk ways)katika hospitali ya Wilaya ya Ikungi katika kijiji cha Mahambe,Kata ya Unyahati ambapo miradi huo kwasasa upo katika hatua ya upasuaji wenye kugharimu kiasi cha Shilingi 194,200,000/-
Mradi huo unafanyika baada ya ukamilishaji wa miradi ya ujenzi wa majengo nane(8) ikiwemo jengo la maabara, kichomea taka,jengo la mionzi,jengo la wagonjwa wa nje,jengo la utawala,Johari ya dawa na jengo la kufulia kupitia bajeti ya Shilingi 350,000,000 kutoka serikali kuu mwaka wa fedha 2023/24.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya wilaya ya Ikungi Dkt.Yesaya Mwandigha amesema kuwa Kukamilika kwa miradi wa njia za kutembelea,(walk ways)utasaidia kuunganisha majengo mbalimbali hospitalini hapo pamoja na kurahisisha kutembea katika njia yenye kivuli bila kupigwa jua wala kunyeshewa mvua kwa wagonjwa na watumishi wa hospitali hiyo huku usafirishaji wa wagonjwa na bidhaa za afya kutoka eneo moja kwenda jingine na kuepusha matumizi ya machela kubeba wagonjwa yakibaki kuwa historia.
Katika kuhakikisha kuwa suala la elimu linapewa kipaumbele,Katibu Tawala Mkoa ameongoza timu hiyo kukagua mradi wa ujenzi wa Nyumba ya waalimu(2 in 1), mabweni mawili,madarasa manne na matundu kumi(10)ya vyoo kwa ajili ya kidato cha tano katika Shule ya sekondari Nkuhi Mtaturu unaogharimu kiasi cha shilingi 454,000,000 kutoka serikali kuu ambapo mpaka sasa ujenzi huo umefikia zaidi ya asilimia 90 ya utekelezaji wake.
Kaimu Mkuu wa Shule hiyo Mwl.Suleman Abeidy amesema kuwa licha ya fedha kutoka serikalini lakini pia wananchi wamekua mstari wa mbele kwa kazi mbalimbali ikiwemo kusafisha maeneo ya ujenzi na kung'oa visiki,kuchimba vichuguu,kujaza vifusi na kuleta maji ambapo thamani ya nguvu zao ni Shilingi 5,718,500/-
Kadhalika Kaimu Mkuu wa Shule amesema moja ya changamoto iliyopo ni miundombinu ya barabara isiyo rafiki inayosababisha shughuli za ujenzi kusimama mara kwa mara kwa vifaa vya ujenzi kutofika kwa urahisi katika eneo la ujenzi.
Hatimaye walitembelea Ujenzi wa Shule ya Msingi na Sekondari Kintandaa ,Kata ya Mtunduru,Tarafa ya Sepuka ambao umefikia asilimia 95 katika utekelezaji wa ujenzi wa majengo yake.
Ujenzi wa Shule hiyo unahusisha ujenzi wa majengo mbalimbali yakiwemo madarasa 8 na ofisi mbili za waalimu,jengo la utawala,maabara ya Kemia,Baiolojia na Fizikia, maktaba, chumba cha TEHAMA,Matundu matano ya vyoo,kuchomea taka na tanki la maji la ardhini.Pia walitembelea ujenzi wa madarasa mawili na vyoo katika shule ya msingi Kintandaa ambapo mradi huo umefikia asilimia 95 ya utekelezaji.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi Bw.Kastori Msigala akizungumza mara baada ya ukaguzi huo amesema watahakikisha wanaweka juhudi kubwa ili miradi hiyo kumalizika kwa wakati na kwa ubora wa hali ya juu ikiwemo kuongeza idadi ya mafundi ili kazi ziweze kukamilika na kukabidhiwa kwa wakati uliowekwa.
Akitoa maagizo mara baada ya ukaguzi wa miradi yote hiyo Katibu Tawala Mkoa wa Singida Daktari Fatuma Mganga,ametoa maagizo mbalimbali ikiwepo kuhakikisha miradi hiyo yote unakamilika na kukabidhiwa ifikapo June 30,2025.Sambamba na hilo ametoa agizo la utunzaji wa mali na mazingira ya miradi kwa ujumla kwa kuhakikisha upandaji wa maua na miti unapewa kipaumbele ili kuwa na mandhari rafiki na utunzaji wa mazingira pia kwa kuhakikisha pia wanakua wabunifu katika utengenezaji wa miundombinu ya kuvuna maji ya mvua.
Kadhalika katika miradi ya ujenzi wa shule ametoa maagizo kwa waalimu kuhakikisha wanainua ufaulu wa wanafunzi wao kwa kiwango cha juu kwani mazingira ya ufundishaji ni rafiki sana kwa sasa ikiwemo majengo mazuri,samani bora,vifaa vya kufundishia na mengineyo hivyo ili kuonyesha mchango chanya kwa Serikali ni vema kuweka juhudi kubwa na ubunifu katika kuwaongezea idadi ya ufaulu ili kuwawezesha kuendelea na masomo ya sekondari na vyuo vikuu pia .
singidars.blogspot.com at 22:25
Share
No comments:
Post a Comment
›
Home
View web version
Powered by Blogger.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.