Halmashauri ya Itigi mkoani Singida imefikia asilimia 88 za anwuani za makazi kwa kuyafikia majengo 30,789 kati ya 35,000 yaliyokuwa yametarajiwa pamoja na uwepo wa changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika utekelezaji wa kazi hiyo.
Akitoa taarifa hiyo leo katika ukumbi wa Halmashauri hiyo Mkurungezi Mtendaji wa Halmashauri hiyo John Mgalula amesema taarifa za makazi zimekusanywa katika Kata 13 za Halmashauri hiyo na kazi ya ukusanyaji na uingizaji wa taarifa katika mfumo unaendelea kwa maeneo yaliyobaki.
Amesema taarifa zilizobaki wanategemea zitakamilika kwa ukamilifu wake ifikapo mwishoni mwa wiki hii ambapo zoezi litakaloendelea litakuwa la kupachika vibao katika mitaa mbalimbali huku vingine vikiendelea kutengenezwa.
Akizitaja baadhi ya changamoto zilizojitokeza katika zoezi hilo Mgalula amesema Upungufu wa fedha za utekelezaji wa zoezi hilo pamoja na umbali wa baadhi ya maeneo pamoja na ukosefu wa mitandao ya simu katika baadhi ya vijiji jambo ambalo limesababisha kupungua kwa kasi ya utekelezaji wa zoezi husika.
Hata hivyo Mkurugenzi huyo amesema Halmashauri imeendelea kukusanya fedha kupitia vyazo mbalimbali vya mapato ili kutatua baadhi ya changamoto zilizojitokeza.
Pamoja na hayo Mkurugenzi akaendelea kuomba ngazi ya Mkoa huo pamoja na Wizara kuangalia changamoto za mfumo ambazo zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara ambazo zimechangia kutofikiwa malengo kwa wakati.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Binilith Mahenge akijibu hotuba ya Mkurugenzi amewapongeza kwa hatua waliyoifikia na kuwataka kuhakikisha wanafikia lengo ifikapo mwisho wa wiki hii ili kuwezesha kukamilika kwa zoezi na kuandaa taarifa ya pamoja ya Mkoa.
Aidha, ameagiza Halmashauri hiyo kufanya mawasiliano ya karibu na chuo cha VETA wilayani hapo ili kupata vibao vya barabarani kwa gharama nafuu huku akiagiza kushirikishwa Idara na taasisi mbalimbali katika upatikanaji wa vibao hivyo.
Awali RC alikagua Mradi wa ujenzi wa shule ya Sekondari Kitaraka ambapo amewapongeza wananchi wa Kata hiyo ambao wamejitolea nguvu zao katika ujenzi wa shule hiyo na kuahidi kwamba atahakikisha kwamba Ruwasa na Tanesco wanafikisha huduma ya maji na umeme kabla ya wanafunzi kuanza masomo.
Mradi huo unahusisha jengo la Utawala lenye thamani Tsh. Milioni 82.8, madarasa manne yenye thamani ya Tsh.Milioni 253.16, Maabara ya kompiuta yenye thamani ya milioni 32.92, Maktaba yenye thamani ya Milioni 56.5, vyumba vitatu vya Maabara vyenye thamani ya Tsh. Milioni 208, matundu 20 ya vyoo yenye thamani ya Milioni 46.8 pamoja na ujenzi wa tanki la maji.
Katika taarifa iliyotolewa na Mkuu wa shule ya Sekondari Itigi Mwl. Jacob Mwabeza imebainisha kwamba ujenzi huo mpaka kumalizika utagharimu kiasi cha Tsh. Million 680.2 na mradi unategemewa kukamilika kabla ya tarehe 28 Mei 2022.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.