Wakuu wa Idara katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama wametakiwa kufanya kazi kwa kushirikiana na kufuata taratibu za kazi ambazo ndizo zitakazoleta mafanikio ambapo wamekumbushwa kwamba lengo la uwepo wao ni kuwaletea maendeleo wananchi husika na sio vinginevyo.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge alipokutana na kufanya kikako cha pamoja na viongozi mbalimbali wakiwemo wakuu wa Idara katika ukumbi wa Halmashauri hiyo ambapo alielekeza Watumishi kufuata taratibu za utumishi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku na kufanya kazi kwa kushirikiana.
RC Mahenge amesema pamoja na kwamba Wilaya ya Mkalama inafanya kazi nzuri ya makusanyo ya mapato lakini bado kuna changamoto zinazosabishwa na usimamizi usioridhisha hivyo kuwataka wakuu wa Idara kuhakikisha wanashirikiana ili kuondoa changamoto za miundombinu ya Barabara, Elimu, Afya, Amani na usalama pamoja na kuhakikisha maendeleo yanatamalaki Wilayani hapo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge akizungumza na Watumishi wakati wa kikao hicho.
Hata hivyo Dkt. Mahenge amewapongeza Viongozi wa Wilaya hiyo kwa hatua ambazo wamezifikia katika kutatua changamoto ndogondogo za migogoro ya mipaka katika baadhi ya maeneo katika Kata ya Mwangezi wanapoishi jamii ya wahazabe na kuwataka kufikia mufaka kwa njia ya majadiliano ili kuhakikisha Amani inaendelea kutawala maeneo hayo.
Awali akitoa taarifa ya moja ya eneo lenye changamoto ya migogoro wa Mipaka Diwani wa Kata ya Mwangeza ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Bosco Charles Samweli amesema Kata yake imekuwa na changamoto ya migogoro ya mpaka baina ya watu jamii ya Wahazabe na wengine wa Mkoa wa Arusha na Manyara jambo ambalo halina Afya nzuri kwa Amani ya Kata hiyo.
Ameiomba Serikali kuendeleza juhudi zake za kutatua changamoto hiyo ambapo shughuli za maendeleo kwa jamii hizo zimesimama wakisubiri majadiliano yanayoendelea baina ya viongozi wa mikoa hiyo.
Aidha Diwani ameomba msaada wa haraka kwa wataalamu wa wanyamapori ili kusaidia kuondoa changamoto ya uvamizi unaofanywa na wanyama pori wakiwemo Tembo na Simba katika mashamba ya wanakijiji ambapo mashamba yao yamekuwa yakiharibiwa na Serikali ilishindwa kulipa fidia kwa wakulima hao.
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Sophia Kizigo akizungumza na Watumishi wakati wa kikao hicho.
Akitolea majibu changamoto hiyo Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Sophia Kizigo amesema Serikali hailipi fidia kwa wakulima bali inalipa kiasi kidogo cha kifuta machozi au pole kwa walikutwa na dhahama ya kuvamiwa na wanyama na kuharibiwa kwa mazao yao.
DC Kizigo amesema kwamba tayari mawasiliano yameshaanza kufanyika ili kusaidia kuwapangia kazi hiyo wataalamu wa wanyamapori ili kukabiliana na changamoto hiyo huku Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo akikiri kutengwa eneo lenye ukubwa wa ekari 10 kwa ajili ya zoezi hilo.
Kikao hicho kilihudhuriwa na wakuu wa Idara na vitengo viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya pamoja na timu kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambapo lengo la kikao hicho ilikuwa ni kuangalia changamoto zinazokabili Kata ya Mwangeza Wilayani hapo.
Mwisho
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.