Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida ameagiza uwajibikaji kwa timu ya uratibu wa afya Mkoa kuhakikisha wanajituma na kufanya kazi kwa weledi ili kuepusha mlipuko wa ugonjwa wa kipindu pindu katika Mkoa wa Singida.
Ameyasema hayo katika kikao kazi cha kujadili namna ya kukabiliana na ugonjwa wa kipindu pindu leo Novemba 22,2024 kilichofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Singida kikiratibiwa na mganga Mkuu wa Mkoa Daktari.Victorina Ludovick.
Akizungumza katika kikao hicho,Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Daktari Fatuma Mganga ametoa maelekezo mbali mbali kwa timu ya uratibu wa afya Mkoa katika kukabiliana na ugonjwa wa kipindu pindu ikiwemo kutibu maji yote yanayotumika vijijini na visima vya watu binafsi majumbani,kuhakikisha kila kaya ina choo cha kutumia,timu kuweka kambi yenye vifaa vya kutosha katika maeneo hatarishi na kuhakikisha shule zote za Msingi na Sekondari Zina vyoo na sehemu za kunawia mikono pamoja na TARURA kuhakikisha wanarekebisha bara bara zote zisizo rafiki kurahisisha ufikiwaji rahisi wa maeneo yenye viashiria vya hatari.
"Kila mmoja wetu hapa ahakikishe anawajibika ipasavyo katika kuunga mkono juhudi za kupambana na kipindu pindu,wadau wote kila mmoja atumie nafasi yake kwa matokeo mazuri ya mpangokazi na kuleta mrejesho wa utekelezaji wa majukumu yake"alisema Daktari Mganga.
Pia amewaagiza kupima sampuli za maji katika maeneo tofauti tofauti ili kubaini visima vyenye vimelea vya ugonjwa wa kipindu pindu ili kuwa rahisi kuyatibu na kuepusha matumizi yake kwa wananchi wa maeneo husika.
Awali akiwasilisha taarifa juu ya ugonjwa wa kipindupindu,Afisa Afya wa Mkoa wa Singida Bw.Sebastian Mgeta,ameainisha visababishi mbali mbali vya ugonjwa huo ikiwemo ukosefu wa maji safi na salama katika maeneo yenye mlipuko,ukosefu wa vyoo katika kaya,baadhi ya kaya kutotumia dawa za kutibu maji,imani potofu na kuchelewa kwenda kupata matibabu pindi tu dalili zinapoonekana.
"Licha ya hayo changamoto za miundombinu ya barabara kutokua rafiki kunachangia kutofikiwa kwa urahisi kwa maeneo yenye viashiria vya ugonjwa huo,usibuaji kutofanyika kikamilifu,wagonjwa kuficha taarifa za ugonjwa na ushiriki hafifu wa baadhi ya viongozi unarudisha nyuma juhudi za kupambana na ugonjwa wa kipindu pindu.alisema Bw.Sebastian.
Pia ameainisha kazi mbali mbali zilizotumika kama njia ya kupambana na ugonjwa huo ikiwemo huduma ya usibuaji katika kaya mbalimbali mgonjwa anapobainika,kuhamasisha jamii kuhusu utumiaji wa vyoo bora na kutoa elimu maeneo mbali mbali,kutibu visima pamoja na vikao vyavujirani mwema kati ya Ikungi,Igunga na Uyuwi.
Akizungumza kuhusu changamoto ya maji katika maeneo yenye mlipuko,Meneja wa RUWASA Mkoani Singida Bw.Lucas Said amesema kuwa shirika lipo katika mikakati ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa visima vya maji maeneo kadhaa kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya mahi safi na yaliyotibiwa.
Katika kikao hicho wajumbe wameazimia kushirikiana kwa pamoja kuepusha mlipuko zaidi wa ugonjwa wa Kipindu pindu huku wakiahidi kuchangia mahitaji mbali mbali yanayohitajika ili kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo hatari.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.