ASKOFU wa Kanisa Katoliki Jimbo la Singida, Mhashamu Edward Mapunda amewahimiza Watanzania kutumia mwaka huu kwa sala na maombi wakati Taifa likielekea kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, huku akiwasihi Wakristo nchini kote kumtumia Mama Bikira Maria ili aweke uchaguzi huo kwenye Moyo wake mtakatifu kwa sababu yeye ni Malkia wa Amani.
Askofu Mapunda aliyasema hayo kupitia mahubiri ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye tukio la uzinduzi wa kituo cha Hija na Maombezi cha Bikira Maria kilichopo katikati ya nchi ya Tanzania eneo la Sukamahela lililopo wilayani Manyoni mkoani hapa.
“Leo ni siku ya Amani Duniani, tukumbuke Yesu Kristo ni Mfalme wa Amani na Bikira Maria ni Malkia wa Amani, hivyo ni lazima tuombe Amani kwa sababu amani ni zawadi toka kwa Mungu. Kupitia kituo hiki tuombee amani familia zetu, mkoa wetu, Taifa na Dunia”. Alisema Mapunda
Akiwasilisha ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisco kwa siku ya Amani Duniani, Askofu Mapunda alisema amani ni safari ya matumaini, majadiliano, upatanisho, uongofu wa mazingira na haiwezi kujengeka kwa vitisho na hofu ya maangamizi.
Alisema amani ya kweli inafumbatwa katika mifumo ya kisiasa, kijamii, na kiuchumi inayozingatia haki na msamaha-huku akisisitiza na kumtaka kila mmoja kujitahidi kuwa chombo cha amani.
Aidha Askofu huyo kwa niaba ya jumuiya nzima ya Kanisa Katoliki nchini amemshukuru na kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi kwa wazo lake la kiufunuo na Takatifu la kuona sehemu hiyo inafaa kuwa mahali sahihi na fursa ya kukutana na Mungu kwanjia ya Bikira Maria.
“Tunamshukuru sana Mkuu wa Mkoa Nchimbi, wazo hili limetoka kwa Mungu kupitia yeye lakini pia Mkuu huyu wa Mkoa ni rafiki wa Mama Bikira Maria, hivyo aliponiletea wazo hili na nilipo tafakari nikaona ni wazo la Mungu na ni ufunuo”. Alisema Mapunda
Pia alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kwa sehemu ya mchango wake muhimu katika kufanikisha ujenzi wa kituo hicho cha hija aliyoutoa hivi karibuni wakati akiwa safarini kuelekea Chato kwa mapumziko.
Akielezea umuhimu wa kituo hicho Mapunda alisema, kituo hicho hakizinduliwi kwa bahati mbaya bali ni zawadi ya Mungu kwa binadamu wote, na kwamba uwepowake utasaidia sana kuimarisha Imani na kuleta chachu ya uinjilishaji…Ni fursa ya Baraka na Neema, pia ni fursa ya kuomba amani na kuimalisha Ibada zetu na Bikira Maria.
“Kituo hiki cha Sukamahela kilichopo Parokia ya Chipumagwa ni cha pili kuzinduliwa baada ya kile cha kwanza kilichopo pale Kimbwi. Kila mwaka mwezi wa tisa tunakutana Kimbwi kujikabidhi kwa Bikira msaada wa daima ili atuombee, lakini ratiba ya kituo hiki cha Sukamahela itakuwa ni kila tarehe 9 Disemba lengo likiwa ni kuombea mkoa wetu amani, Taifa na Dunia”. Alisema Mapunda
Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Nchimbi, alisema kila Mtanzania anapaswa kuwa shahidi juu ya ushuhuda wa wazi usio na mashaka kuhusu upendo mkubwa na uwajibikaji wa Bikira Maria kwa ulinzi, ulezi, maombezi na usalama wa Taifa.
Nchimbi alikiri kwa kutoa mfano wa uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2015, uchaguzi uliojaa misukosuko, hofu na mashashaka, wasiwasi na hata wengine walitamani kuikimbia Tanzania, lakini kilichotuvusha sio kingine bali ni Mama huyu mkingiwa dhambi ya asili, Mama wa Kristo, Bikira Maria.
“Ndio maana mama huyu hatimaye leo hii amesimama katikati ya nchi hii hapa Sukamahela ili kuendelea kutuvusha kwa amani, tusichoke kumkimbilia, tusichoke kumuomba ili taifa letu daima likapate kuwa na amani kupitia maombezi yake”. Alisema Nchimbi
MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.