Wanasheria wabobezi zaidi ya 40 kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Wizara ya Katiba na Sheria na wa Mkoa wa Singida wataweka kambi ya siku tano katika kliniki ya sheria bila malipo kwa lengo la kutoa ushauri wa kisheria kwa wananchi, watumishi wa umma na viongozi mkoani hapa.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe.Halima Dendego, amezungumza hayo leo Mei 16,2025 na waandishi wa habari wakati akitambulisha uzinduzi wa Kamati ya Ushauri wa Kisheria ngazi ya Mkoa ambayo itafuatiwa na uendeshaji wa kliniki ya sheria bila malipo kwa wananchi wote wa Mkoa wa Singida kuanzia Mei 19 hadi 23 mwaka huu.
"Namshukuru Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kulinda, kukuza na kutetea haki za wananchi wanyonge na kupinga vitendo vya uvunjifu wa haki za kibinadamu,misingi ya utawala wa sheria, ukatili wa kijinsia na kuheshimu utawala wa sheria ambao ndio msingi wa maendeleo," amesema Mhe.Dendego.
Mhe.Dendego amesema Kamati za Ushauri wa Kisheria za Mikoa na Wilaya zimeanzishwa kwa mujibu wa sheria ya utekelezaji wa majukumu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali sura ya 268 na mwongozo wa huduma za ushauri wa Kisheria katika ngazi ya Mkoa na Wilaya.
Amesema faida za kamati hizo za mikoa na wilaya ni kupunguza mashauri au migogoro dhidi ya serikali,huduma za ushauri wa kisheria ambazo zitakutanisha mawakili wa sheria wa taasisi mbalimbali na kuwasaidia wananchi wenye changamoto mbalimbali.
Mkuu wa Mkoa amesema kuwa faida nyingine ni uwepo wa huduma ambao utawawezesha mawakili wa serikali kusimamia utawala wa sheria katika maeneo yao,kupunguza malalamiko ya kisheria kutoka kwa wananchi, kutoa elimu ya sheria kwa umma katika kushughulikia changamoto mbalimbali na kupunguza vitendo vya uonevu na vinavyovunja sheria na taratibu.
"Nitoe rai kwa wananchi wote kujitokeza kwa wingi siku ya uzinduzi pamoja na kuhudhuria kliniki ya kisheria kuanzia Mei 19 hadi 23 na wakati wote wa kliniki kutakuwa na Kamati ya Ushauri wa Kisheria ngazi ya mkoa,Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mawakili wa Serikali kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali," amesema Mhe.Dendego.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Sheria Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Matrider Meckson, amesema siku ya uzinduzi kutakuwa na wanasheria wabobezi kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Wizara ya Katiba na Sheria na wa kutoka Mkoa wa Singida.
"Tumelenga kupunguza mashauri kwasababu kuna malalamiko mengi na pia tunataka kuhakikisha tunapunguza mashauri yanayoenda mahakamani pamoja na wananchi kuhakikisha wanapata haki zao," amesema.
Meckson alisema wanasheria hao wabobezi ambao watakuwa zaidi ya 41 watahakikisha shauri au malalamiko ya wananchi yanafuatiliwa hadi mwisho na ufumbuzi kupatikan hivyo wenye malalamiko mbalimbali ikiwemo ya ardhi,mirathi nakadhalika.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.