Huduma ya Mahakama Mtandao itatekelezwa kwa ufanisi mkubwa nchi nzima kwa sababu Serikali imewekeza katika ujenzi wa miundombinu ya elimu ambayo ilionekana kuwa kikwazo katika utoaji na usimamizi wa haki na masuala ya kisheria.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Binilith Mahenge leo Februari 2, 2022 wakati akitoa salamu kwa Mawakili mbalimbali na wananchi waliohudhuria kilele cha siku ya sheria iliyofanyika ki Mkoa katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa Singida.
Dkt. Mahenge amesema kwamba Serikali imewekeza vyumba vya madarasa zaidi ya elifu 15 nchi nzima huku akiutaja mkoa wa Singida kwamba wamepata madarasa 632 ambapo Sekondari ni 330 na Msingi yakiwa 332 jambo ambalo limesaidia watoto wote kupata nafasi ya kwenda shule.
Aidha Rc Mahenge akaendelea kueleza kwamba kitendo cha watoto wote kwenda shule kitasababisha kiwango cha elimu kuongezeka jambo ambalo litasaidia kuongeza uelewa na kurahisisha matumizi ya huduma Mahakama mtandao.
Kwa sasa Serikali imeendelea kuviwezesha vikundi mbalimbali kujiajiri ikiwa ni pamoja na kuvipatia mikopo ya asilimia 10 ambapo vijana hao wataweza kumiliki mitaji na vifaa vya mawasiliano ambavyo huduma za kisheria za kimtandao zitapatikana.
Naye Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Ally Nzowa wakati akitoa hotuba yake ameshukuru Serikali kwa ujenzi na ukarabati wa Mahakama za Kisasa zenye mifumo ya teknolijia za kisasa sehemu mbalimbali hapa nchini ili ziendane na mazingira ya utoaji haki.
Amesema wanasheria wanajivunia uanzishwaji wa Mahakama zinazotembea ambapo zimesaidia utoaji wa huduma za kimahakama hasa katika mji wa Dar es salaam na Mwanza ambapo zaidi ya watu 1,500 wamehudumiwa.
Hata hivyo Mhe. Nzowa akaendelea kuiomba Serikali kuboresha miundombinu kama uwepo wa umeme wa uhakika, ili huduma hiyo iweze kutolewa maeneo mengi zaidi.
Akiendelea kuyataja mafanikio ya Mahakama Hakimu akasema kila hakimu amepatiwa kompiuta mpakato ambazo zinawasaidia kuchapa hukumu, kufanyia mikutano kwa njia ya video na kwamba uwepo wa huduma ya Mahakama mtandao pamoja na Mahakama inayotembea kumesaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa Mahakama alifafanua Mhe. Nzowa.
Mkuu wa Ofisi ya Mashtaka wa Mkoa wa Singida Mhe. Juma Salige pamoja na shukrani akaiomba Serikali hasa kipindi hiki ambacho Mahakama zinafanya mabadiliko makubwa ya kiutendaji kuongezewa bajeti kwenye Mahakama, Polisi na Magereza kwa kuwa wanategemeana ili kuongeza ufanisi.
“Mahakama imekuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi kupitia utoaji wa haki na usimamizi wa sheria jambo ambalo likiratibiwa vizuri litaleta manufaa makubwa kwa nchi”. Alisema Juma Salige.
Awali akiwawakilisha Mawakili wa kujitegemea katika kilele cha maadhimisho hayo Wakili Peter Njingo akaiomba Serikali kuielimisha jamii kwa upana ili kurahisisha utoaji wa huduma za kisheria kwa kuwa wananchi wengi wamekuwa wakishindwa kuendeleza kesi zao kwa sababu ya ufahamu mdogo wa matumizi ya teknolojia za simu Janja.
Akiendelea na hotuba yake Wakili Peter akaishauri Serikali kuingiza mafunzo ya Mahakama mtandao katika mitaala ya vyuo ili Mawakili waweze kujifunza kabla hawajaingia makazini kwa kuwa changamoto ya matumizi ya Mahakama mtandao ni ya watu wote.
Hata hivyo wakili huyo akasisitiza Serikali ikutane na makampuni ya simu kama Tigo, Airtel, Hallotel Vodacom na TTCL waweze kukubaliana kupunguza gharama za mabando ya intaneti ili wananchi waweze kupata misaada ya kisheria kupitia mitando. .
Akimalizia hotuba yake Wakili huyo akaiomba Mahakama kuongeza idadi ya maafisa TEHAMA katika Mahakama ili kutoa msaada wa kiufundi mara zinapotokea changamoto za mifumo ili huduma ziweze kuendelea na malengo kufikiwa.
Wawakilishi wa wananchi na baadhi ya viongozi wa Dini katika siku ya kilele cha siku ya sheria ambayo ilikuwa na kauli mbiu ya “Zama za mapinduzi ya nne ya viwanda, safari ya maboresho kuelekea Mahakama ya mtandao”.wakaguswa na kutoa maoni yao ambapo Askofu wa Kanisa la Anglikana Mkoa wa Singida John Lupaa akahidi kutoa magodoro 50 kwa ajili ya wafungwa waliopo katika Gereza la Manyoni .
Askofu amesema alipata fursa ya kulitembelea na kujionea changamoto inayowakabili wafungwa hao hivyo kuiomba jamii kutoa msaada wa kisheria na mali kwa kila anayeguswa.
Akiwawakilisha wananchi Bwana Saidi Sombi ambaye alitumia Sanaa ya ushairi kupeleka ujumbe wake amebainisha kwamba matumizi ya TEHAMA katika mahakama yameongeza uwazi, uwajibikaji wa watumishi na imeleta unafuu kwa wananchi ambao walikuwa wakishindwa kufuatilia kesi zao kwa sababu ya umbali au kutokuwa na muda wa kutosha.
Viongozi Meza Kuu wakishiriki wimbo wa Taifa mara baada ya kuwasili uwanjani
Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskasi Muragili akizungumza kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Singida
Meza Kuu ikiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Dini mkoa wa Singida
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.