Wataalamu wa afya Mkoani Singida wametakiwa kupunguza vifo vya wakina mama wajawazito na watoto kwa kuimarisha matumizi ya mfumo wa M-Mama unaotekelezwa pembezoni mwa miji na kuhakikisha uwepo wa vifaa tiba vitakavyotumika kuwahudumia wazazi pindi watakapopelekwa hospitalini.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatma Mganga wakati wa kikao cha tathimini ya mfumo wa M-Mama kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kanisa Katoliki Wilayani Manyoni.
RAS Fatma amewataka Wakurugenzi kuendelea kuhamasisha wananchi wa vijijini kutumia mfumo kwakuwa takwimu zinaonesha kwamba zipo Halmashauri ambazo hawajatumia fedha yeyote kulipa madereva jamii jambo ambalo amesema ni kinyume na utaratibu wa utekelezaji wa mfumo.
Akizitaja Halmashauri ya Manyoni, Singida DC na Manispaa ya Singida ambapo kwenye mfumo inaonesha matumizi kidogo ya mfumo na wengine wakiwa hawajatumia kabisa huku akieleza kwamba mfumo ni moja ya afua ya kupunguza vifo vya wakina mama na watoto hivyo watendaji wa vijiji washirikishwe katika kusaidia utekelezaji wa mfumo.
"Tulitarajia kuona idadi ya wagonjwa wanaoletwa na gari la wagonjwa kwenye Hospitali zetu yangekuwa kidogo ikilinganishwa na dereva jamaii jambo linalothibitisha kwamba huenda elimu haijatolewa kwa wananchi". Dkt. Fatma
Hata hivyo RAS Mganga akatoa maelekezo kwa waganga wakuu wa Wilaya kuhakikisha mfumo unafanya kazi na madereva jamii wanalipwa ndani ya siku saba baada ya kutoa huduma na kusimamia uwepo wa vifaa tiba muhimu ili isiwe mgonjwa kaletwa ili afie hospitalini.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu Mkoa wa Singida, Elikana Lubango alieleza kwamba mkutano huo umelenga kufanya tathimini na kujadili changamoto mbalimbali ambazo zimetokea katika utekelezaji.
Hata hivyo alieleza kwamba zipo Halmashauri ambazo zimekuwa na matumizi kidogo sana ya fedha kwenye mfumo na nyingine zikiwa hazijatumia kabisa hivyo kikao hicho ameeleza kwamba kitatumia kupata maelezo ya kina kwamba kwa nini hapakuwa na utekelezaji.
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi, Kelvin Ferline kutoka Pathfinder International Singida amesema Mkutano huo utatoa mwanga katika kuyafikia malengo yaliyokusudiwa huku akisisitiza uhamasishaji kufanyika Vijijini na kuongeza usajili wa madereva jamii kama sehemu ya kupata huduma.
Hata hivyo Afisa Maendeleo ya Jamii ambaye alimuwakilisha Mkurugenzi wa Wilaya ya Manyoni wakati akimkaribisha mgeni rasmi amesema katika Mkutano huo wanakwenda kuweka mpango kazi utakaonesha namna ya kupambana na changamoto zilizojitokeza.
Kikao hicho kilihudhuriwa na waganga wakuu wa Wilaya zote pamoja na kamati za Afya.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.