Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, amesema kuwa Maafisa Maendeleo ya Jamii lazima wajipime kwa matokeo wanayoyaleta kwa wananchi na si kwa idadi yao au vikao wanavyohudhuria, akisisitiza kwamba kazi yao kuu ni kuifikia jamii na kuleta mabadiliko chanya.
Akizungumza katika kikao kazi cha Maafisa Maendeleo kutoka wilaya zote za Mkoa wa Singida kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mhe. Dendego amesema amefurahi kukutana nao kwa sababu ndiyo msingi mkubwa wa mafanikio ya wananchi katika ngazi ya jamii.
“Nimefurahi kukutana nanyi kwa sababu tuna mambo mengi ya kuyajadili ili kuhakikisha tunatekeleza mipango mbalimbali ya serikali na huduma zinawafikia wananchi. Tuhakikishe tunawafikia wananchi na tunawaelimisha, kwani haitakuwa na maana huduma hizi hazitawafikia,” amesema RC Dendego.
Ameeleza kuwa Maafisa Maendeleo wanapaswa kujitathmini kama kweli wanatekeleza wajibu wao ipasavyo na kuleta tija, badala ya kukaa maofisini wakisubiri wananchi wawafuate. “Ukiitwa Afisa Maendeleo, kila eneo linakuhusu. Tupimane kwa malengo yetu ili tulete tija kwa wananchi wetu,” amesisitiza.
Pia,Mkuu wa Mkoa amesema anaifahamu vyema taaluma hiyo kwa kuwa yeye mwenyewe ni mwana sayansi wa jamii, hivyo anajua namna ilivyo na jukumu kubwa katika kubadilisha tabia na ustawi wa wananchi.
“Sisi tunahusika moja kwa moja na kurekebisha tabia za jamii, tunawajenga raia wema wa taifa hili,” amesema.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa Maafisa Maendeleo kuviunda vikundi, kuvisimamia, kuvilea na kuvifikisha kwenye taasisi za fedha, ili wanawake, vijana na watu wenye ulemavu waweze kupata mikopo na kujikwamua kiuchumi. “Tija sio uwingi wetu, tija ni namna tunavyoipeleka jamii mbele kwa vitendo,” amesema.
Ametumia kikao hicho kuwataka Maafisa Maendeleo waamke na waone kama wanatimiza malengo ya serikali.
“Tupate ndoto ya kuwatoa wananchi wa Singida hapa walipo, tusibaki kusema hiki ni kikao kazi bila vitendo. Hiki ni kikao cha operation, kama kumponya mgonjwa, tupate suluhisho. Swali kubwa ni: namna gani mnaifikia jamii? Tuache kukaa tu ofisini, tufike field.”
Kadhalika Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Daktari Fatuma Mganga amesema kuwa kikao hicho pia kina maazimio kadhaa cha kuhakikisha wanakwenda kujitathimini juu ya kwamba ni namna gani wameweza kuwafikia wananch na yapi ni matokeo ya wao kuwepo maeneo hayo ikiwa ni kuhakikisha wananchi wanaishi mazingira bora ikiwemo kuwa na vyoo bora,ukatili dhidi ya wanawake na watoto,mikopo ya wanawake na walemavu,fursa mbalimbali za wananchi kuwekeza,kadhalika dawati la huduma za msaada wa kisheria ikiwa ni kwa namna gani wanatumia jukwaa hilo kuhakikisha wanashighulikia kero za wananchi na mengineyo mengi.
"Tunalo jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa yale ambayo tumekasimiwa na Mhe.Rais,Wakurugenzi na viongozi wengine katika ngazi ya Wilaya tunayafanyia kazi na yanaleta matokeo ili nasisi tuonekane kuwa tunafanya kazi yenye matokeo chanya katika jamii"amesema Daktari Mganga.
Kadhalika amesema kuwa moja ya azimio la kikao hicho ni kuhakikisha Maafisa hao wanakwenda kushuhulikia suala la marejesho ya fedha zote ambazo vikundi mbali mbali vilikopa ikiwemo mikopo ya asilimia kumi kwa lengo la kuhakikisha inawafikia wengine ambao hawajapata kadhalika kusimamia vema vikundi vilivyopo ili kupiga hatua kubwa zaidi za kiuchumi.
Kauli hizo zimekuja wakati Maafisa Maendeleo wakiwa kwenye mkutano wa pamoja kujadili changamoto zilizopo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, mikataba ya vikundi pamoja na namna ya kuhakikisha wanavifikia vikundi vyote vya jamii kwa usawa.
Ni katika majadiliano yao, Maafisa Maendeleo wamejadili changamoto zinazohusu utekelezaji wa kanuni mbalimbali ikiwemo mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, pamoja na mikataba ya vikundi vya kukopeshwa ili kuhakikisha malengo ya serikali ya kuwainua kiuchumi makundi haya muhimu yanafanikiwa ipasavyo.
Kikao hicho kimetoa fursa kwa Maafisa Maendeleo kubadilishana uzoefu na kuja na mikakati ya pamoja itakayosaidia kuharakisha maendeleo katika jamii za Mkoa wa Singida.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.