Madiwani wametakiwa kuacha mzaha wa kuwachekea na kuwaendekeza watumishi ambao wamesababisha Halmashauri ya Wilaya ya Iramba kupata hati chafu ya Mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za Serikali katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi ameyasema hayo jana wakati wa baraza maalum la madiwani la kujadili hoja 122 za mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za serikali katika halmashauri hiyo.
Dkt Nchimbi amewaambia madiwani kuwa wao ndio wazawa na ndio wawakilishi wa wananchi hivyo wanapozembea kuwasimamia na kuwabana watumishi ili wafuate kanuni, sheria na miongozo, watakaoumia ni wananchi wao pamoja na halmashauri yao kukosa ruzuku ya serikali.
“Madiwani acheni mzaha wa kuwachekea hawa watumishi, unapoona hoja ujue kiwanda ni watumishi, lakini mmepata hati chafu miaka mitatu mfululizo hamshtuki tu kuna watu wana wanawahujumu? Au mnaweza kujiendesha bila ya ruzuku ya serikali? Semeni leo? Wananchi wamewaamini hebu watumikieni ipasavyo,” amesema Dkt Nchimbi.
Ameongeza kuwa halmashauri inapoendelea kupata hati chafu hiyo ni sifa mbaya kwao na hata kwa mkoa mzima kwakuwa watendaji wa ngazi za mkoani mpaka halmashauri wanaonekana wameshindwa kutekeleza wajibu wao vema.
Dkt Nchimbi amesema madiwani waweke utaratibu ili wakuu wa idara waliothibitishwa wabaki katika halmashauri hiyo kwa kipindi kirefu kwakuwa wamekuwa wakithibitishwa kisha wanahama jambo linalowafanya wakose wakuu wa idara wa kutosha na kubaki na wanaokaimu.
“Kuna baadhi ya watumishi wanaharibu tu kwakuwa wanajua watahama hapo, lakini ninyi madiwani na wananachi hamtaweza kuhama hapo ndio kwenu hivyo basi wekeni utaratibu tu, mkuu wa idara akithibitishwa abaki hapo kwa muda awatumikie wananchi au akitaka kuhama basi atafute wa kubadilishana naye”, amesisitiza.
Aidha Dkt Nchimbi amewataka watumishi kuacha uzembe, watumie fursa zilizopo katika kujiongezea kipato lakini wasifanye biashara na halmashauri huku akiwashauri kuwasikiliza viongozi wa dini ambao wanawahimiza uadilifu na uchapa kazi.
Naye Mkaguzi wa Nje wa Hesabu za Serikali Annamary Kakunguru amesema baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo wamekuwa wazito katika kujibu hoja, kufuta hoja pamoja na kufuata maoni ya mkaguzi wa Nje hivyo kuisababishia halmashauri kuwa na hoja nyingi zinazodumu kwa muda mrefu.
Kakunguru amesema watumishi wanapaswa kubadilika na kuwa na utendaji mzuri pamoja na kupeana ushirikiano ili kwa pamoja waweze kufuta hoja na kuweka mikakati mizuri ya kuzuia hoja.
Pia Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt Angelina M Lutambi amewaasa watumishi kufanya kazi kwa kufuata miongozo, sheria na kanuni ili kuepuka kutengeza hoja huku wakuu wa idara wanaokaimu wakitakiwa kufanya kazi kwa bidii ili utendaji wao uonekane.
Lutambi ameongeza kuwa utendaji wa ushirikiano ndio utaifanya halmashaur hiyo kusonga mbele huku akiwaeleza kuwa hoja za mkaguzi wa hesabu za serikali zinawakumbusha kuongeza uadilifu na usimamizi wa fedha na shughuli za serikali.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Iramba Linno Mwageni amemshukuru Dkt Nchimbi kwa kuwakumbusha kuwajibika ili waendane na kasi ya awamu ya tano ya hapa kazi tu.
Mwageni amemweleza Mkuu huyo kuwa siku nyingine asisite kuwaonya pale wanapoenda tofauti huku akiahidi kwa niaba ya watumishi kubadilika na kuongeza bidii katika utendaji na usimamizi wao.
Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amekabidhi kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli vitanda vya kuzalia vitatu, vya kawaida 20, mashuka hamsini na magodoro hamsini vyenye thamani ya shilingi milioni 25 kwa hospitali na vituo vya kutolea huduma za afya Wilayani humo.
Dkt Nchimbi amesema Rais Magufuli ameonyesha upendo wake kwa wana Iramba hivyo wasiogope kutumia huduma za afya katika vituo vya serikali kwa kuwa sasa huduma zimeboreshwa, huku akiwaasa wakunga wa jadi wawaache wajawazito wakajifungulie hospitali na vituo vya afya.
Ameongeza kuwa watoa huduma na madaktari sasa wameboreshewa mazingira ya kufanyia kazi hiyo wanapaswa kutoa huduma kwa uadilifu mkubwa na kwa bidii.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Iramba Boniphace Richard amemshukuru Rais Magufuli kwakuwa walikuwa na upungufu wa mashuka 400, ambapo jitihada za Rais zimewapatia mashuka 150 huku wakipanga kununua mashuka 200 kwa mapato ya ndani.
Jitihada za Rais Magufuli zimeungwa mkono na Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Katibu Tawala wa Mkoa, Mwenyekiti wa halmashauri na madiwani, Mkurugenzi wa halmashauri na watumishi ambao kwa pamoja wamechangia mashuka 96, magodoro matano na pesa shilingi elfu hamsini.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.