Wilaya za Manyoni na Ikungi katika Mkoa wa Singida zinatarajiwa kupokea mabilioni ya fedha kutokana na utunzaji wa misitu ya asili vikiwamo vichaka vya Itigi (Itigi Thickets) ambavyo ni adimu duniani na katika Bara la Afrika vinapatika Tanzania na Zambia pekee.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mheshimiwa Halima Dendego, amesema hayo wakati wa maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara ambayo yaliadhimishwa kwa viongozi wa chama, serikali na wananchi kupanda miti 501 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida.
Kabla ya zoezi la kupanda miti katika hospitali hiyo kufanyika, Dendego aliongoza viongozi wa chama, serikali na wananchi kutembelea katika wote za wagonjwa kuwapa faraja na kuwapa zawadi mbalimbali.
Mhe.Dendego Amesema mkakati mwingine uliopo ni kutengeneza mpango wa matumizi ya ardhi, kuendelea kuhifadhi misitu ya asili kwani misitu ni fedha kutokana na biashara ya hewa ukaa yenye faida nyingi na Mkoa wa Singida utakuwa miongoni mwa wanufaika wa fedha hizo.
“Wilaya yetu ya Manyoni na Ikungi ipo mbioni itaanza kupokea mabilioni ya fedha muda mchache ujao, niwapongeze wakuu wa wilaya kwa kupambana maana wananchi wetu wakiona kitu ndo wataamini, miti yetu ni dhahabu ya kijani,” alisema.
Dendego alisema mkoa utaendelea na zoezi la kuhamasisha upandaji miti zoezi rasmi la upandaji litafamnyika Januari 2025 na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kunusuru misitu.
“Vipo vijimisitu vya asili au vichaka vya Itigi, Manyoni na Ikungi, tunaviona kama ni maeneo hatarishi lakibi kumbe ni mazalia ya tembo,yaani tembo anapotaka kuzaa ndo anakwenda kwenye vile vichaka,” alisema.
Awali Afisa Maliasili Mkoa wa Singida, Charles Kidua alisema miti 13,399,031 ambayo ni kati 33,253,602 iliyopandwa katika Mkoa wa Singida katika kipindi cha kuanzia 2019 hadi 2024 imekufa kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo utunzaji hafifu.
“Katika uhifadhi wa misitu na mazingira mkoa umepanda jumla ya miche ya miti 33,253.602 sawa na asilimia 63 ya lengo kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita na miti iliyopona ni 19,854,571 sawa na asilimia 59.7 ya miti iliyopandwa,” alisema.
Kidua alisema sababu za miti mingi inayopandwa kufa ni kutokana na uharibifu unaofanywa na mifugo, utunzaji hafifu,mchwa kuharibu miche, kuwepo kwa vipindi virefu vya jua na uelewa mdogo wa wananchi juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Alisema katika kipindi hiki cha mvua miti 1,768,192 imepandwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Singida ambapo mkoa utaendelea na zoezi la upandaji miti ipatayo 5,395,909 katika vyanzo vya maji,taasisi za serikali,watu binafsi na taasisi za kidini hadi mwisho wa msimu huu wa mvua.
Kidua alisema katika kuhifadhi mazingira mkoa umejiwekea dira na mwelekeo kwa kuongeza utekelezaji wa upandaji miti kutoka asilimia 63 ya sasa mpaka asilimi 90 ifikapo 2030 na kuongeza idadi ya misitu ya hifadhi kufikia hekta 100,000 ifikapo 2030.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.