Wananchi wa Manispaa ya Singida wametakiwa kuhifadhi takataka wanazo zalisha majumbani mwao badala ya kuzitupa barabarani au kuzipeleka kwenye majalala huku Halmashauri ya Manispaa hiyo ikiagizwa kuweka utaratibu wa kupita kila kaya kukusanya taka hizo.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa huo Peter Serukamba alipokagua Majalala ya soko la Kibaoni, Kindai, Akwa na uwanja wa Ndege kujionea hali ya usafi ambapo mengine yapo katika makazi ya watu.
Amesema hali ya usafi katika Manispaa hiyo hairidhishi kwa kuwa majalala yamekuwa mengi katika makazi ya watu na kukaa muda mrefu bila kuzolewa hivyo kutishia usalama wa afya za watu wa maeneo hayo.
Hata hivyo ilielezwa kwamba Manispaa hiyo haina vifaa pamoja na magari ya kuzolea taka jambo ambalo linasababisha uchafu kukaa kwa muda mrefu katika majalala hayo.
Kutokana na mazingira hayo RC Serukamba amatoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Jeshi Lupembe kwamba kila mwananchi ahifadhi taka zake nyumbani kwake na Manispaa wazunguke kukusanya taka hizo kwa kila kaya ambapo watastahili kuchangia.
Aidha amemtaka Mkurugenzi kuongeza nguvu kwenye kukusanya fedha kupitia wazalishaji wa taka ambapo ndani ya kipindi kifupi watapata fedha za kununua vifaa vya ukusanyaji kutokana na ushuru huo wa taka.
Hata hivyo amemueleza Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida Yagi Kiaratu kuhakikisha kwamba vikao vya Baraza ya Madiwani wanatunga Sheria kali ya kuzuia utupaji wa taka na faini kwa atakayekamatwa akifanya hivyo.
Mwisho
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.