Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amewataka wawekezaji wa Viwanda vya kuchakata mafuta ya kula mkoani Singida, kuhakikisha wanaimarisha uhusiano kati yao na wakulima, na kuingia mikataba yyenye tija kwa ajili ya kilimo, ili kuongeza uzalishaji wa zao la alizeti, kukidhi mahitaji ya mafuta ya kula nchini.
Akizungumza baada ya kujionea maendeleo ya ujenzi wa kiwanda kikubwa, cha kukamua mafuta ya alizeti, kinachomilikiwa na Kampuni ya Wild Flower Grain and Oil Mills, na kingine cha Mount Meru, Mkoani Singida, Naibu Waziri Kigahe amesema kuwa, ili kuongeza upatikanaji wa mbegu za mafuta ya alizeti, ni lazima mbinu mbalimbali ziweze kutumika, ikiwemo kuimarisha uhusiano na wakulima wote wa Mkoa wa Singida, na maeneo mengine nchini, yanayolima zao hilo.
Aidha Naibu Waziri amefafanua kuwa, licha kutumia njia hiyo, pia Wamiliki hao wa Viwanda watafanikiwa zaidi iwapo watasaidia na kuliwezesha kundi la vijana, kwa kuwapatia mashamba makubwa, ili kujikita kwenye shughuli za kilimo cha alizeti, hivyo kuongeza upatikanaji wa zao hilona kuweza kukidhi mahitaji ya Viwanda.
Amesema Serikali imeboresha na kuimarisha upatikanaji wa mbegu Bora za alizeti, na kuwapatia wakulima mbolea kwa bei ya ruzuku, hivyo ni lazima pawepo na jitihada za makusudi, kuweza kuongeza uzalishaji wa zao la alizeti na mengine kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa Wananchi, hususani wakulima wa Mkoa wa Singida.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Singida ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhe.Godwin Gondwe, amesema kubwa msimu huu wa kilimo Mkoa wa Singida umepokea mbegu Bora ya zao la alizeti kutoka wakala wa Taifa mbegu za kilimo Tani 307, amabazo zimesambazwa kwa wakulima, ili kuongeza upatikanaji wa zao la alizeti, msimu ujao.
"Mheshimiwa Naibu Waziri, tayari mbegu hizo zimewafikia wakulima mapema zaidi, ili hatimaye waweze kuotesha alizeti na kumaliza tatizo la mafuta ya kula hapa nchini, ambalo hulilazimu Taifa kutumia fedha nyingi, kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi,"alifafanua Mhe.Gondwe.
Kwa mujibu wa ofisi ya kilimo mkoa, mbegu hizo ni sehemu ya mahitaji ya Tani 2,000 zilizoombwa serikalini, kwa ajili ya kumudu kupandwa kwenye ekari zaidi ya milioni moja Mkoani Singida, lengo likiwa ni kuipunguzia mzigo Serikali kwa kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.
Naibu Waziri Kagahe, yupo kwenye ziara ya siku tatu mkoani Singida iliyoanza Februari 18, kwa ajili ya kutembelea na kukagua Viwanda, Migodi na shughuli nyingine mbalimbali, zinazotekelezwa na Serikali, pia wawekezaji wa ndani na nje, ili kuchochea kasi ya ukuaji uchumi kwa jamii.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.