Mkuu wa Mkoa wa Singida,Mhe Halima Dendego amewatembelea na kufanya mkutano na wanufaika wa mfuko wa kunusuru kaya masikini TASAF na kusikiliza kero na maoni mbali mbali waliyonayo katika Kata ya Itigi Mjini,ikiwa ni muendelezo wa ziara yake katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi.
Miongoni mwa malalamiko aliyopokea ni kuondolewa kwa idadi kubwa ya wazee katika unufaika wa TASAF walioomba serikali iwarudishe wapate huduma hiyo kwani ni ngumu kwa wao kuweza kumudu gharama za maisha na kujitegemea ili kujiingizia kipato kwani utendaji kazi wao umepungua sana na afya zao kutokua imara kutokana na umri kusogea.
Akijibu kero hiyo,Mkuu wa Mkoa ametoa maagizo kwa waratibu wa TASAF kuhakikisha wanafanyia kazi suala hilo kwa kuwarejesha wale wote wanaostahili katika mfuko huo na kuhakikisha malipo kwa wale ambao hawajapata fedha zao ndani ya muda wa miezi miwili kushughulikiwa kwa wakati.
Pia,alizindua mradi wa ujenzi wa zahanati ya Kashangu,Kata ya Idodyandole,zahanati Iliyoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi na mwishowe kuungwa mkono na serikali na kukamilika kwa asilimia mia moja.
Awali akisoma taarifa ya mradi,Kaimu Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kashangu,Twahil Amdan amesema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia watu zaidi ya 3200 kutoka katika maeneo ya Kashangu na maeneo ya jirani kupata huduma za afya bila kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo.
Akizungumza na wananchi baada ya kuzindua mradi huo,Mkuu wa Mkoa amewaagiza wahudumu wa afya kuzingatia huduma bora kwa kuhakikisha wazee,wajawazito na watoto wachanga chini ya miaka mitano wanapatiwa huduma bila malipo.Pia ameomba kuongezwa kwa wakunga wenye uzoefu wa muda mrefu kazini ili kuboresha na kutoa huduma bora na ya uhakika zaidi hasa katika masuala ya uzazi.
Pia ameahidi kutatuliwa kwa changamoto za uhaba wa maji ya kutosha katika eneo hilo,umeme,nyumba za watumishi na vyoo vya wafanyakazi kama miongozo inavyoelekeza.
Kupitia mradi huo,wananchi wataepukana na adha ya kusafir umbal mrefu kufuata matibabu,kusaidia wakina mama wajawazito kupata huduma wakati wa ujauzito na kujifungua,kurahisisha upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango,chanjo na ufuatiliaji wa karibu wa makuzi ya watoto chini ya umri wa miaka mitano.Pia utapunguza idadi ya wakina mama wanaojifungulia nyumbani au kwenda zahanati wakiwa katika hatua za mwisho za kujifungua.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.