Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Jerry Silaa,amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuhakikisha anaupandisha hadhi mnara uliojenga katika kijiji cha Hika kata Makuru wilayani Manyoni ili wananchi waweze kupata mtandao wa intaneti wa 3G hadi 4G.
Ametoa agizo hilo leo wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Hika katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tano mkoani Singida baaada ya kuzindua mnara wa mawasiliano ya simu uliojengwa na serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) uliojengwa kwa Sh.milioni 272.
"Kati ya maelekezo aliyonipa Rais wakati akiniapisha ni kuhakikisha wananchi wanapata mawasiliano, namwelekeza Katibu Mkuu ahakikishe kwa haraka sana mnara huu unapandishwa hadhi na unapata mtandao wa 3G na 4G ili wananchi nao waweze kupata intaneti," alisema
Naye Meneja wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL),Agustino Mwakyembe amesema ujenzi wa mnara huo wenye urefu wa mita 60 ulianza kufuatia kusainiwa kwa makubaliano Machi 16, 2021 na ujenzi wake kukamilika Juni 15, 2022.
Amesema mradi huo wenye thamani ya Sh.milioni 272 unatumia teknolojia ya 2G ambao unawezesha wananchi kupiga na kupokea simu za sauti huku wakitumia ujumbe mfupi kwa wakati mmoja (sms).
"Kama sehemu ya dhamira yetu ya kimkakati ya kuimarisha muunganisho katika maeneo ya vijijini tunafanya uboreshaji mkubwa wa minara ya mawasiliano inayofanya kazi sasa kwenye teknolojia ya 2G hadi 4G," alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, amesema uzinduzi wa mnara huo ni muhimu sana katika kata ya Makuru na Wilaya ya Manyoni katika kukuza maendeleo na upatikanaji wa huduma muhimu kama vile elimu,afya na biashara na hivyo kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Mhe.Dendego amemuahidi Waziri kuwa umeme utafikishwa katika mnara huo ili uendelee kufanya kazi kwa ufanisi huku wananchi zaidi ya 24,000 wa eneo hilo wakitegemea kunufaika
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.