Mkuu wa Mkoa wa Singida,Mhe.Halima Dendego amefanya ziara ya ukaguzi miradi na kusikiliza kero za wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi,Kata ya Rungwa,Kalangali,Mwamagembe na Mitundu iliyoanza siku ya Jumanne Novemba 4,2024
Hayo yamejumuisha ukaguzi wa miradi mbali mbali ikiwemo ukaguzi wa zahanati mpya ya Itumba,ukaguzi wa nyumba za watumishi,kukagua mradi wa ujenzi wa Sekondari mpya ya Kalangali katika ziara hiyo.
Miongoni mwa kero zilizowasilishwa na wananchi ni uchache wa watumishi na vitendea kazi mashuleni na katika taasisi za afya,uhitaji wa umeme na maji,barabara,mahitaji ya mbolea na mbegu za ruzuku.Pia malipo ya wakati kwa watumishi na usikivu wa Redio katika maeneo hayo yenye usikivu hafifu yaliwasilishwa na wananchi ili kutatuliwa na Mkuu wa Mkoa.
Akizungumza na wananchi katika maeneo tofauti,Mkuu wa Mkoa Mhe.Halima Dendego ameahidi utatuzi wa kero hizo mbali mbali kwa wananchi ikiwemo kero ya umeme katika maeneo hayo na kuagiza utekelezaji wake ndani ya siku saba katika kata ya Rungwa katika eneo la Sekondari.
Pia,amewaagiza maafisa kilimo kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi kuhusu suala la mbegu,pembejeo,dawa za kuua wadudu na mbolea za ruzuku ili kuwapa uelewa juu ya suala hilo na kuwashauri wananchi kujiandikisha katika daftari la pembejeo za kilimo ili kuweza kufaidika na huduma hizo zenye gharama nafuu kwa kusambazwa na mawakala na vyama vya msingi.
"Nitoe rai kwa wananchi kujiandikisha katika daftari la kilimo bure kabisa bila malipo ili kuweza kupata huduma ya mbegu,mbolea za ruzuku,viuatilifu pamoja na pembejeo kwa bei nafuu kabisa kwa maendeleo makubwa ya kilimo."alisema Dendego
Sambamba na hilo,Mkuu wa Mkoa ameagiza utekelezaji imara wa Shule ya Sekondari Mpya ya Kalangali iliyopo katika hatua za awali za ujenzi,huku akitoa muda kwa wahusika wa ujenzi wa nyumba ya mtumishi na zahanati ya Itumba kuhakikisha inakamilika katika viwango bora zaidi kuliko ilivyo sasa.
"Serikali imewekeza fedha nyingi katika kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi hususani katika utoaji wa fedha za kutosha za ujenzi wa nyumba za watumishi na zahanati pia,hivyo ni jukumu letu kuhakikisha zinajengwa kwa ubora wa hali ya juu zinazosadifu gharama zinazotolewa"alisema Mhe.Dendego.
Charles Clement Mgama na Stephano Minja wananchi kutoka kata ya Rungwa ni miongoni mwa wananchi walifurahia ujio wa Mkuu wa Mkoa wa Singida katika wilaya ya Itigi wakisema wana imani kubwa kuwa changamoto zao zinakwenda kupatiwa ufumbuzi wa kero mbali mbali.
"Ujio wa Mkuu wa Mkoa utaleta ufumbuzi katika changamoto zetu nyingi ikiwepo changamoto ya umeme,maji,barabara,utatuzi wa migogoro ya ardhi,watumishi na nyinginezo kwani tunaamini zimefika kwa mtu sahihi ambaye ni daraja kati yetu na serikali kuu"alisema Mgama.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.