Kufuatia muendelezo wa wiki ya huduma kwa wateja,Viongozi na watumishi wa Bank ya NMB wametembelea ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida kwa lengo la kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi popote pale walipo.
Mkuu wa mkoa wa Singida,Mhe.Halima Dendego akizungumza katika hafla hiyo amesema ni wakati wa Mkoa wa Singida kukua katika matumizi ya huduma za kibenki kwa kuboresha na kuwafikia wananchi wengi zaidi katika huduma za kibenki hususani kwa wananchi wa vijijini katika maeneo ya uzalishaji hivyo ni wakati wa kufanya utafiti ili kigundua maeneo ya uzalishaji na yenye mzunguko mkubwa wa kifedha ili kupeleka huduma maeneo hayo kwa kuongeza idadi ya mawakala na mashine za ATM.
Dendego amesema Kwa kufanya hivyo,uzalishaji utaongezeka maradufu kutokana na upatikanaji na mzunguko wa fedha kuwa rahisi na usalama wa wananchi utaongezeka kwani wataepuka kuhifadhi ela ndani na kutumia njia rahisi za kibenki katika utunzaji wa fedha zao.
"Ni vyema tuainishe maeneo mbali mbali yanayohitaji kufikiwa na huduma za kifedha mjini na vijijini ili kupeleka huduma karibu na wananchi kwa lengo la kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla kwani mzunguko wa fedha utakua mkubwa na uzalishaji utaongezeka"alisema Dendego.
Katibu tawala Mkoa wa Singida,Daktari Fatuma Mganga,amesema ni wakati wa wananchi kunufaika na huduma za kibenki hususani kwa wananchi wa vijijini wanaojishuhulisha na uzalishaji kwa kufunguliwa akaunti na kupewa elimu juu ya matumizi ya huduma za kibenki.
Pia amesisitiza elimu ya huduma hizo kutolewa katika vikundi mbali mbali ikiwemo vikundi vya wanawake, vikundi vya mikopo ya Halmashauri ,wakulima na wafanyabiashara ili kuwapa utayari wa kuthubutu kutumia huduma za kibenki zenye gharama nafuu na usalama wa kutosha.
Naye Meneja wa Benki ya NMB mkoani Singida,ameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa kuhakikisha wanayafikia maeneo yote ya Mkoa wa Singida katika kuhakikisha wanafikiwa na huduma za kifedha mahali popote na wakati wowote kwa kuongeza idadi ya mawakala wakubwa mjini na vijijini pia uwepo wa ATM zitakazorahisisha upatikanaji wa fedha kwa urahisi na usalama zaidi.
Mikakati hiyo ni moja ya njia za kukuza na kuongeza matumizi ya kibenki katika mkoa wa Singida ambao ni moja ya mikoa yenye matumizi madogo ya huduma hizo hapa nchini.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.