Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amemwagiza Mkandarasi wa Kampuni ya HAINAN kutoka CHINA kuhakikisha anafanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha ujenzi wa daraja la mto SIBITI ambayo linaunganisha mikoa ya Singida na Simiyu ili kuondoa adha kubwa wanayopata wananchi hasa kipindi cha mvua.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo mapema leo alipokuwa Mkoani Singida wakati anaweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Daraja la mto Sibiti baada ya kutoridhika na maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo ambalo limechukua zaidi ya miaka sita licha ya mkandarasi kulipwa zaidi ya asilimia 90 ya gharama za ujenzi wa daraja hilo ambalo ujenzi wake unagharimu shilingi za kitanzania bilioni 16.
Rais MAGUFULI pia amewataka watendaji wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kumsimamia ipasavyo mkandarasi huyo ili aweze kukamilisha ujenzi huo kabla ya mwezi wa TATU mwakani na kama mkandarasi atashindwa kukamilisha kazi hiyo kwa muda ulipangwa basi atachukua hatua zaidi dhidi ya wahusika akiwemo mkandarasi huyo.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwele amesema ujenzi wa daraja la Mto Sibiti utakuwa ni mkombozi mkubwa kwa Wananchi wa mikoa ya Singida na Simiyu katika uimarishaji wa shughuli za kiuchumi kwenda ukanda huo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi kwaniaba ya wananchi wa Mkoa wa Singida amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli pamoja na Serikali ya awamu ya Tano kwa kuifanyia mambo mengi ya kimaendeleo mkoani hapa."Serikali imetupatia jumla ya shilingi za kitanzania bilioni ishilini na nne katika masuala ya Elimu ya kuwezesha Elimu bure kwa Wananchi, ukarabati wa miundombinu ya shule, ujenzi wa hosteli na mikakati mingine ya Elimu Bure, hizi ni fedha nyingi na zimefanya mambo makubwa sana mkoani Singida."
"Tumepokea pikipiki 136 kwa ajili ya waratibu wa elimu za Kata na tayari zimeshagawanywa na sehemu zingine zinaendelea kugawanywa. Pia tumepokea fedha za ujenzi wa vituo vya Afya ambavyo ni 10 pamoja na fedha za kutandaza nguzo za umeme vijijini. Hii ni Singida njema sana." Dkt. Nchimbi.
Aidha, Wananchi wa mikoa ya Singida na Simiyu wamemshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kwa ujenzi wa daraja hilo ambalo kwa kupitia Serikali ya Awamu ya Tano imeweza kutoa shilingi za kitanzania bilioni 16 ili Wananchi wake waweze kunufaika kwa miundombinu bora ya barabara ambapo kwa ujenzi huo wa daraja litasaidia kuongeza na kuimarisha uchumi. "Tunamshukuru Rais Magufuli kwa kuweka jiwe la msingi la daraja hili na hii inaonyesha jinsi gani Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano, Dkt. John Magufuli anavyotekelea kwa vitendo ILANI YA CCM kwani daraja hili litakuwa mkombozi kwetu wananchi wa Singida na Simiyu pamoja na wananchi kutoka pande za Tanzania kwani hapa kuna shughuli nyingi sana za kibiashara hususani CHUMVI hupatikana kwa wingi sana na kwa bei rahisi" Wananchi Sitibi.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.