Ucheleweshaji wa fedha na malipo kidogo kwa vibarua na mafundi yanayolipwa na wakandarasi katika miradi ya ujenzi wa nyumba ya kuhifadhia maiti (Mochwari) pamoja na wodi ya wanawake na wodi ya wanaume zinazojengwa katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida umechangia ucheleweshaji wa ukamilishwaji wa mradi huo jambo ambalo viongozi wameagiza kukomeshwa hali hiyo.
Akiongea baada ya ukaguzi wa majengo hayo na kusikiliza malalamiko ya baadhi ya vibarua na mafundi ambao walilalamikia kutolipwa fedha zao kwa wakati na kulipwa ujira mdogo, Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatma Mganga leo amezitaka kamati za ujenzi kukutana na mkandarasi wa majengo hayo na kuwalipa madeni yao kwa vibarua na mafundi wanaofanya kazi hiyo pamoja na kukaa mezani na kukubaliana malipo mapya ili kuondoa migomo baridi ya vibarua hao.
Aidha RAS amesema kwamba hayupo tayari kuona fedha za Seriki zinarudi hazina mwisho wa mwaka wakati miradi ya maendeleo ya wananchi haijakamilika hivyo kumuelekeza Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo Furaha Mwakafwila kukutana na Mkandarasi huyo na kuona kama inawezekana kuachia jengo moja kwa mafundi wengine ili kazi ziweze kukamilika kwa wakati.
"Kila fundi anatakiwa kuwalipa vibarua wake kwa wakati na stahili walizokubaliana tofauti na hivyo itakuwa ni sababu ya ucheleweshaji wa kazi, na tulishatoa maelekezo kwamba fundi mmoja jengo moja kama inawezekana Mkandandarasi ashauriwe awaachie mafundi wengine jengo moja"
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya Furaha Mwakafwila amemuahidi Katibu Tawala huyo kwamba watakutana na Makandarasi kujadili namna ya kuboresha hali ujenzi, malipo ya vibarua na kuhakisha kazi inakamilika ndani ya wakati.
Hata hivyo RAS alitembelea Mradi wa Ujenzi wa shule ya Eka iliyoko Kata ya Eka Wilayani Manyoni chini ya Mradi wa Boost unaogharimu jumla wa Milioni 493.4 wenye vyumba vya madarasa 14 na Awali viwili na jengo la Utawala ambapo amewataka watendaji wa vijiji na kata kuhamasisha wananchi kuchangia nguvu kazi lengo likiwa fedha zilizotolewa zinatosheleza.
Hata hivyo RAS Dkt. Fatma ametoa maagizo kwa wasimamizi wa ujenzi wa miradi ya boost Mkoani hapo kuhakikisha mafundi wanakuwa na mipango kazi katika eneo la kazi itakayoonesha namna ya utekelezaji wa shughuli za kila siku tofauti na hivyo mafundi wataonekana wanafanya kazi kila siku lakini majengo hayaendelei.
Hata hivyo RAS amesema Serikali kwa kiasi kikubwa imetambua umuhimu na mchango wa mafundi wa mtaani ndio maana imeendelea kuwapa kazi hivyo kuwataka kutopoteza imani hiyo kwa kufanya kazi nzuri, kutofanya uharibifu wa vifaa vya ujenzi na kubakiza kazi kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Awali RAS amewaeleza walimu katika miradi hiyo kuhakikisha wanapanda miti ya kivuko na matunda maeneo yanayowazunguka ikiwa ni pamoja na kuyapendezesha maeneo kwa kutengeneza bustani za maua.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.