Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego, mapema leo (Septemba 27, 2024) amekutana na Watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba lengo kuu likiwa ni kuboresha utendaji kazi wa watumishi katika halmashauri hiyo ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Akizungumza kwenye kikao kazi kilichofanyia katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Iramba, RC Dendego amewataka Wakuu wa Idara na Vitengo katika halmashauri hiyo kuhakikisha wanasimamia miradi yote ya maendeleo ili kukamilika kwa wakati, ubora na kwa thamani ya fedha pasipo kuzalisha madeni.
"Serikali inapoleta fedha za ujenzi wa mradi inakuwa imeshapiga mahesabu ya kukamilisha sasa ninashangaa iweje halmashauri nyingine mradi huohuo umekalimika kwa thamani ya fedha iliyoletwa nyie hamjakamilisha au umekamilika ila mmezalisha madeni, sitaki kusikia jambo hilo" RC Dendego
Mkuu huyo wa Mkoa amewasisitiza watendaji hao wa halmashauri kwa kila mkuu wa Idara kuweka mpango kazi wake kwa kufuata Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inavyoelekeza kwa kuhakikisha kuwa yale yanayotakiwa na ilani hiyo yanatekelezwa kikamilifu.
Aidha, katika kikao kazi hicho RC Dendego, amewaelekeza maafisa elimu wa halmashauri hiyo kuhakikisha wanapandisha hali ya taaluma kwa kiwango cha juu na kukomesha utoro wa wanafunzi kwa kuwa elimu ni msingi wa maendeleo ya taifa.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga, akisisitiza jambo kwenye kikao kazi hicho.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa huyo amewahimiza watendaji hao kushirikiana kikamilifu katika ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya halmashauri akisema bila mpango wa kifedha unaoeleweka haiwezekani kufanikisha malengo ya halmashauri.
Akizungumza na Idara ya Utumishi amesema inawajibu wa kusimamia haki za watumishi na kuhakikisha kuwa masuala ya kiutumishi yanashughulikiwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na matumizi bora ya teknolojia katika kurahisisha shughuli za kiutumishi.
Hata hivyo, RC Dendego, ametumia kikao hicho kuwataka Wakurugenzi wa Halmashauri mkoani humo kutowahamisha watumishi bila idhini ya Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) ili kudhibiti uhaba wa watumishi na kuweka uwiano bora katika utoaji wa huduma.
Pia RC Dendego, amewaagiza wakaguzi wa ndani katika halmashauri hiyo kuwa macho na kutoruhusu dosari zozote kutokea bila kuchukua hatua akisema kuwa hataki kusikia kwamba kuna jambo limegundulika lakini halijaripotiwa au kushughulikiwa.
Kwaupande wa Idara ya Afya RC Dendego, amewaagiza wahudumu wa afya kuongeza uangalizi wa hali ya juu pindi wanapokuwa kazini hasa wakati wa kutembelea wodi kujua changamoto za wagonjwa ili kutoa huduma bora.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa huyo alihitimisha kwa kuwaonya viongozi kuwa hataki kuona halmashauri inarudi nyuma katika utekelezaji wa majukumu na maendeleo hususan katika usimamizi wa miradi, elimu, mapato huku akiwataka walimu na maafisa taaluma kuhakikisha kuwa wana mipango inayotekelezeka kwa manufaa ya elimu.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.