Mkuu wa Mkoa wa Singida Mheshimiwa Halima Dendego, leo ametembelea mabanda ya maonesho ya Nanenane ya Kimataifa yanayoendelea jijini Dodoma.
Katika ziara yake, Dendego alijionea na kupongeza ubunifu na maendeleo mbalimbali yaliyowasilishwa na washiriki kutoka mikoa na taasisi mbalimbali nchini.
Mkuu wa Mkoa huyo aliwahamasisha wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi kushiriki na kujifunza kutoka kwenye maonesho haya muhimu.
Alisisitiza umuhimu wa maonesho ya Nanenane katika kuhamasisha maendeleo ya kilimo, ufugaji na uvuvi, akieleza kuwa ni fursa muhimu kwa wakulima na wadau wengine katika sekta ya kilimo kubadilishana ujuzi na teknolojia mpya zinazoweza kuboresha uzalishaji na kuongeza tija.
"Maonesho haya ya Nanenane ni jukwaa muhimu la kukuza na kuimarisha sekta ya kilimo nchini. Rai yangu kwa wananchi hususan wakulima na vijana kuendelea kujitokeza kwa wingi ili kupata elimu na mbinu bora zitakazowasaidia kuboresha maisha yao kupitia kilimo," alisema Dendego.
Ziara ya Mhe. Dendego ilipokelewa kwa furaha na washiriki wa maonesho hayo ambao walimweleza mafanikio wanayopata kupitia ushiriki wao katika maonesho ya Nanenane 2024 pamoja na maboresho.
Pia alitembelea mabanda ya teknolojia ya kilimo uendelezaji wa mbegu bora na bidhaa za chakula zilizoongezwa thamani akionyesha kufurahishwa na ubunifu unaoendelea katika sekta hiyo.
Maonesho ya Nanenane ya Kimataifa ni tukio la kila mwaka linalowaleta pamoja wakulima, wafugaji, wavuvi, watafiti, na watoa huduma mbalimbali ili kubadilishana maarifa na teknolojia zinazolenga kuboresha kilimo na sekta nyingine zinazohusiana.
Maonesho hayo yanayoendelea kufanyika jijini Dodoma yamevutia washiriki wengi kutoka ndani na nje ya nchi.
Mkuu wa Mkoa huyo ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Maandalizi ya Maonesho hayo ya Kimataifa amewashukuru Viongozi mbalimbali kwa kutembelea maonesho hayo yanayoendelea jijini Dodoma.
Dendego alimalizia kwa kusema uwepo wa Viongozi hao katika maonesho hayo ni ishara kubwa ya ushirikiano na dhamira ya Serikali katika kuendeleza sekta ya kilimo nchini.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.