Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego, ameagiza Halmashauri zote mkoani humo kuhakikisha mikopo ya asilimia 10 inawafikia walengwa hadi vijijini ikiwa ni pamoja na akina mama, vijana, watu wenye ulemavu, na wazee ili kuimarisha uchumi wa wananchi na kusaidia maendeleo hadi ngazi za vijiji.
RC Dendego ametoa agizo hilo kwenye mkutano wa Programu ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi "IMARISHA UCHUMI NA MAMA SAMIA (IMASA)" iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano RC Social uliyopo Singida Mjini Octoba 3, 2024.
Mkuu wa Mkoa huyo, amewataka vijana kuachana na tabia ya kutumia muda wao kwenye michezo ya pool table na badala yake wachangamkie fursa zinazotolewa na mifuko ya uwezeshaji kiuchumi pamoja na mikopo ya asilimia 10 ya halmashauri, ili waweze kujikwamua kiuchumi.
RC Dendego, amewasisitizia wakinamama na walezi kutowakumbatia vijana wenye umri wa zaidi ya miaka 18 ambao bado wanakaa nyumbani bila kujishughulisha akieleza kuwa wengi wao hupelekea kujihusisha na vitendo vya uhalifu.
Kwaupande wake, Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga, amepongeza na kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuridhia mikopo ya asilimia 10 kupatiwa makundi ya akinamama, vijana, watu wenye ulemavu na wazee huku akiwataka kutumia fursa za mikopo hiyo kwenda kuanzisha viwanda vidogo vya uzalishaji nishati mbadala akisisitiza kuwa hatua hii itachangia katika kukuza uchumi wa mkoa na kuboresha maisha ya wananchi.
Ameeleza kuwa nishati mbadala ni muhimu katika kuimarisha maendeleo endelevu na kupunguza utegemezi wa nishati ya kawaida.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.