Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge leo amekabidhi pikipiki 166 kwa Maafisa Ugani wa Halmashauri za Mkoa huo kama sehemu ya vitendea kazi na kuwataka kufanya mabadiliko makubwa kwenye sekta ya kilimo na ufugaji huku akisisitiza upatikanaji wa takwimu sahihi kwakuwa itakuwa rahisi kuwafikia wakulima walipo.
Akizungumza kabla ya kukabidhi pikipiki hizo Dkt. Mahenge amesema pikipiki 161 zitakabidhiwa kwa Maafisa Ugani wa Halmashauri za Manyoni, Singida Dc, Iramba, Ikungi, Itigi, Mkalama na Manispaa ya Singida huku pikipiki 5 zikigawiwa kwa Maafisa Ushirika wa Mkoa huo ambapo zitatumika kuwafikia wakulima pamoja na vyama vya Ushirika katika kuleta tija kwenye Kilimo.
Aidha Dkt. Mahenge ameeleza kwamba msimu wa kilimo unaokuja Serikali inampango wa kugawa mbegu za alizeti kwa wakulima kama ilivyofanya kwa msimu uliopita hivyo akawaagiza Maafisa Ugani hao kuimarisha usimamizi wa kilimo ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo ambayo yatachangia pato la wakulima na taifa kwa ujumla.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge akizungumza na Maafisa Ugani, Maafisa Ushirika pamoja na viongozi mbalimbali wa Halmashauri za Mkoa wa Singida wakati wa hafla ya makabidhiano ya pikipiki iliyofanyika nje ya Ofisi ya Mkuu wa MKoa wa Singida
“Niishukuru sana Serikali ya awamu ya Sita kwa jinsi inavyoendelea kutatua changamoto, imeweka msukumo mkubwa kwenye kilimo ili kupata matokeo makubwa, naamini vifaa hivi vitatusaidia kututoa sehemu moja kwenda sehemu nyingine”. RC Mahenge
Amesema, sifa ya mkoa wa Singida ni kilimo na ufugaji ambapo mazao mbalimbali yanastawi yakiwemo alizeti, pamba, mahindi, vitunguu, parachichi hivyo ujio wa pikipiki hizo kutasaidia kufanya mapinduzi ya kilimo kwa kuwa wakulima watafikiwa kwa wakati na kupata elimu stahiki alisistiza RC Mahenge.
Hata hivyo RC Mahenge akawaasa Maafisa Ugani hao kutumia vitendea kazi hivyo kwa umakini na kwa malengo yaliyokusudiwa ili kurejesha thamani yake na kuleta matokea makubwa kwa wananchi huku akionya kutotumika katika biashara binafsi.
Akimalizia hotuba yake akasisitiza maafisa hao kwenda kwenye vyuo vinavyotoa elimu ya udereva ili kuwapata uelewa mpana wa uendeshaji na kuzijua alama za barabarani pamoja na kupata leseni kwa ajili ya usalama wao na chombo husika.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dorothy Mwaluko akisisitiza jambo kwa Maafisa Ugani, Maafisa Ushirika pamoja na viongozi mbalimbali wa Halmashauri za Mkoa wakati wa hafla hiyo.
Naye Natalia Mosha Afisa Kilimo kutoka Halmashauri ya Singida akiishukuru Serikali kwa kuwapatia pikipiki hizo huku akiahidi kwamba wataweza kuwafikia na kuwahudumia wakulima wengi kwa muda mfupi jambo ambalo litaleta matokea makubwa katika sekta hiyo.
Baadhi ya Maafisa Ugani pamoja na Maafisa Ushirika wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge (hayupo pichani) wakati wa hafla hiyo.
Muonekano wa pikipiki hizo.
Mwisho
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.