Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge leo ameliapisha Baraza jipya la ardhi la wilaya ya Mkalama baada ya viongozi hao kuteuliwa na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili kushughulikia migogoro mbalimbali ya ardhi wilayani hapo.
Akiongea baada ya kuwaapisha, RC Mahenge akawataka wajumbe hao kuanza kazi kwa kusoma mihutasari yote ya mabaraza ya nyuma ili waweze kupata uzoefu kabla ya kuanza kutatua kesi zinazowakabili wananchi wa Mkalama.
Aidha amelitaka Baraza hilo kufanya kazi kwa weledi mkubwa katika kuendesha kesi za ardhi na kufanya maamuzi ya busara pamoja na kuepuka vitendo vya rushwa, zawadi na takrima kwa kuwa vinaweza kuathiri maamuzi sahihi ya baraza.
Hata hivo RC Mahenge akatoa malekezo kwa baraza hilo kuhakikisha wanapunguza au kuondoa kabisa kero na migogoro ya ardhi kwa kuhakikisha wanasikiliza pande zote na kuyatembelea maeneo yenye changamoto badala ya maelezo peke yake huku wakikumbushwa kutofautisha kesi za mashamba au ardhi na kesi za wizi wa aina yeyote ile.
“Mfanye maamuzi baada ya kujiridhisha kwa sababu kesi za ardhi nyingi zimekuwa ni za kifamilia lakini pia kuna tofauti kubwa kati ya kesi za mashamba au ardhi na kesi za wizi wa kuku, ninaomba mjifunze kwa wenzenu mshirikiane na vyombo mbalimbali mtakavyoona vinaweza kusaidia lakini mhakikishe haki inatamalaki Mkalama”. Alisema RC Mahenge.
Akimalizia hotuba yake Mkuu wa Mkoa akalitaka Baraza hilo kutafuta namna ya kutatua changamoto ya ardhi kwa vijana kwa sababu familia zinapoingia katika migogoro ya hiyo wanaoteseka na kuingia hasara ni Vijana .
“Nyuso zenu zinaonesha nyie ni watu waaminifu na wenye weledi mkubwa hivyo katika kutekeleza majukumu yenu mapya mfikirie njia nzuri ya kuwasaidia vijana ambao wamekuwa wakiathirika sana na migogoro ya aridhi hasa ile ya kifamilia”. Alisema RC Mahenge.
Mwisho wa Hotuba yake RC Mahenge akabainisha kwamba ardhi ni sehemu nyeti kwa wanadamu na wanyama hivyo kazi hiyo inaweza kusaidia ustawi wa jamii au kuharibu kabisa ambapo alielekeza kwamba utatuzi wa migogoro ufanyike kwa weledi mkubwa .
Naye DC wa Mkalama Sophia Kizigo akilipongeza baraza hilo kwa kupata uteuzi huku akieleza umuhimu wake katika kutatua matatizo ya wananchi wa Mkalama ambao wengi wao wamekuwa wakipoteza haki zao kwa kushindwa kusafiri umbali mrefu kusikiliza kesi zinazohusu ardhi zao.
Amesema wananchi wa Mkalama walikuwa wanalazimika kwenda mpaka Wilaya ya Iramba Mkoani hapo kusikiliza mashauri yao kwa kuwa huko ndipo baraza la ardhi lilipokuwa likipatikana na kulitaka kurejesha Imani za wananchi hao ambao haki zao zilipotea.
Aidha DC Kizigo akaeleza kwamba kiapo walichopata ni ulinzi kwao ambapo wanatakiwa kuepuka kupokea rushwa na kuhakikisha hawachonganishi wananchi .
Hata hivyo DC huyo akamalizia hotuba yake kwa kuahidi ushirikiano mkubwa kwa baraza hilo huku akikumbusha kwamba litapimwa utendaji wake kwa kipindi kisichozidi miezi sita na kuona kama linawasaidia wananchi kutatua migororo au inaongezeka.
Awali akitoa salamu zake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mkalama James Mkwega pamoja na pongezi kwa baraza hilo akawataka kumtanguliza Mwenyezimungu katika shughuli zao ili aweze kuwangoza katika kutatua matatizo ya ardhi ambayo yamekuwa mengi wilayani humo.
Mwenyekiti Mkwega akaendelea kueleza kwamba kazi kubwa imefanyika ya kupata baraza hilo ambapo kilikuwa ni kilio cha Madiwani wote kutokana na malalamiko ya wananchi kupoteza haki zao .
Kupata baraza ni jambo moja na huduma za baraza ni jambo la pili, ni matumaini yetu sisi wanamkalama kwamba huduma yenu itatusaidia kupata haki zetu, James Mkwega.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa baraza hilo Baraka Shuma kwa niaba ya wajumbe akatoa shukrani kwa kuteuliwa katika nafasi hiyo huku akiahidi kutekeleza majukumu yao kwa weledi mkubwa ili kuhakikisha wanawasaidia wananchi wa wilaya hiyo.
Shughuli hiyo ya uapisho ilihudhuriwa na Mkuu wa mkoa Singida, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, viongozi mbalimbali wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba na Mweyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo ambapo Wajumbe walioapishwa ni Charles Jilangi, Kitundu Emanuel Kitundu, Hamisi Igimbi Salum na Zulfa Suphian Mvungi.
Mwisho
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.