Taasisi za umma zilizopo Mkoani Singida zimetakiwa kuwa na kawaida ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma wanazozitoa ili kuondoa kero ambazo nyingine zimetokana na kutoelimishwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kutoa mirejesho kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge wakati akitatua kero za wananchi katika Mikutano ya hadhara iliyofanyika Kijiji cha Mitundu na Itigi katika Wilaya Itigi Mkoani hapo.
RC Mahenge amesema kwamba kero zilizotolewa na bàadhi ya wazee kuhusu kutonufaika na mfuko wa maendeleo ya Jamii TASAF zinatokana na kutowaelimisha vya kutosha au kutorudisha mrejesho baada ya vikao kadhaa vya kujadili majina yao kama utaratibu unavyotakiwa, jambo ambalo alimtaka Mratibu wa TASAF wa Halmashauri ya Itigi kushughulikia swala hilo na kuleta majibu ndani ya muda mfupi.
Hata hivyo RC Mahenge amemtaka Afisa Tawala wa Wilaya ya Manyoni kuwakutanisha bàadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mitundu ambao wanagombania mipaka ya viwanja na wengine wakizulumiana mifugo huku akitakiwa kuandaa kitabu cha malalamiko na namna alivyozishugulikia.
Aidha RC amefutilia mbali utaratibu uliyokuwa ukitumika na watendaji wa Itigi wa kuwapata vijana waliotakiwa kupata ajira za muda katika kazi za wakandarasi wa Barabara na reli kwa kuwa haukuwa na uwazi na haukutumia utaratibu wa ushindani.
Amesema hata kama kuna vijana ambao walishachagulia amewafuta na kumtaka mkuu wa Wilaya kuandaa utaratibu mpya ambapo fomu zitagawiwa kwa idadi inayofaa kwa kila kata na kufuata utaratibu wa ushindani ili kila mtu apate kwa Haki.
RC Mahenge ameahidi kutembelea eneo la hifadhi ambalo limedaiwa kuwa na Madini ya dhahabu lakini wananchi wa Mitundu wakikatazwa kuchimba huku wakidai wageni wameshapewa vibali jambo ambalo amesema Serikali inaendelea na utafiti kwa kushirikisha wadau mbalimbali kuona kama hakutakuwa na athari endapo Madini hayo yakichimbwa ndani ya Hifadhi.
Awali akifungua Mkutano katika Mkutano wa hadhara Kijiji cha Mitundu Mwenyeki wa kijiji hicho Peter Jackson Mkowa akatumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa kuwaletea mbegu ya alizeti ambayo iliuzwa kwa Bei ya ruzuku ya Tsh.3500 kwa kilo moja.
Aidha Mkowa aliomba Serikali kuwaletea mbolea kwa kuwa nayo imekuwa Bei ya juu lakini pia haipatikani kwa wingi jambo ambalo RC Mahenge alitolea maelezo kwamba litafanyiwa kazi hivyo kuwataka wakulima kujiunga katika Ushirika kwa kuwa kupitia huko wanaweza kununua mbolea hata kama Serikali haitatia mkono wake.
Kero zilizotolewa ni kuhusu Barabara za TARURA TANROAD kuweka Alama za x katika nyumba ambako Barabara za mchepuko hupita, malalamiko mengine yakiwa ni ya ugawaji wa ardhi, uwepo wa wanyama waharibifu wa mazao, Tanesco, TTCL na Mpango wa TASAF hoja ambazo ziliweza kutolewa ufafanuzi na wakuu wa Taasisi hizo.
Ziara hiyo inaendelea katika Wilaya ya Manyoni.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.