Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba amemsaidia Bi. Asha Athumani Ibrahimu (53) kupata kiwanja chake alichosumbuka nacho kwa muda wa miaka 25 baada ya kiwanja cha awali kuuzwa na Manispaa ya Mkoa huo.
Akiongea akiwa ofisini kwake RC Serukamba amesema alipata barua kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan ikimuelekeza kuangalia tatizo la mama huyo ambaye amesumbuka nalo kwa muda mrefu hivyo kuwataka Manispaa ya Singida kumpatia mama huyo kiwanja kingine ili kufidia eneo lake lililouzwa kwa mtu mwingine.
Aidha, Mwanamke huyo wakati akikabidhiwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba hati ya kiwanja kipya alichopewa baada ya kusota miaka 25 aliangua kilio kwa furaha katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Asha amepewa kiwanja chake kipya kilichopo eneo la Unyankindi Manispaa ya Singida baada ya Rais kuuagiza uongozi wa Mkoa wa Singida apewe kiwanja kingine baada ya kile cha awali alichokuwa akikimiliki kihalali na kulipia kodi ya ardhi miaka minne mfululizo kuuziwa muuguzi mmoja.
Alisema alibaini kiwanja chake namba 217 kitalu B kuuzwa mwaka 1997 alipokwenda kumwaga kokoto, mchanga na mawe kwa ajili ya kuanza ujenzi ambapo alielezwa na maafisa ardhi kuwa kiwanja chake kimemilikishwa mtu mwingine na kumwahidi kumpatia kingine ndani ya muda mfupi.
Alisema alianza kufuatilia suala hilo kwa viongozi mbalimbali wa Manispaa ya Singida, Wilaya ya Singida na mkoa lakini alikuwa akipewa ahadi tu tangia Juni 2019 hadi ilipofika 4 Aprili, 2022 alipoamua kwenda Ikulu Chamwino jijini Dodoma kwa lengo la kuonana na Rais.
Alisema kufika kwake Ikulu ingawa haikuwa rahisi na hakufanikiwa kuonana na Rais ana kwa ana lakini wasaidizi wake walimsikiliza na hatimaye kutoa maagizo kwa viongozi wa Serikali ya Mkoa wa Singida kushughulikia suala hilo haraka.
Asha alisema katika miaka yote 25 ambayo amekuwa akifuatilia haki ya kiwanja chake amekumbana na changamoto nyingi ikiwamo kupata ajali ya gari mwaka 2016 ambapo alivunjika mguu ambao sasa amekuwa mlemavu hawezi kutembea vizuri.
Aliongeza kuwa pamoja na kupewa kiwanja kingine ambacho akisotea kwa miaka 25 lakini sasa hana uwezo wa kujenga kutokana na kupata ulemavu na kuwaomba wasamalia wema wamsaidie ili apate sehemu ya kuishi.
Aidha, alimshukru Rais Samia na viongozi wa Mkoa wa Singida kwa kumsaidia hadi kupata kiwanja kipya.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akizungumza wakati akimkabidhi hati ya kiwanja kipya alichopewa, alisema alipata barua kutoka ofisi ya Rais ikitoa maelekezo Asha apewe kiwanja kingine baada ya kile cha awali kupewa mtu mwingine.
Alisema baada ya kupata barua hiyo alikaa na viongozi wa Manispaa ya Singida ambao walikiri kiwanja cha Asha alichokuwa akikimiliki kihalali kupewa mtu mwingine.
Serukamba alisema baada ya hapo aliwaagiza viongozi wa Manispaa ya Singida kumtafutia kiwanja kingine haraka Bi.Asha katika eneo atakalopenda yeye agizo ambalo limetekelezwa.
Mkuu huyo wa Mkoa alimwagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida, kupeleka kokoto, mawe na mchanga katika kiwanja kipya alichopewa Asha kwa kuwa kile cha awali alichouziwa mtu mwingine kilikuwa na vitu kama hivyo.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.