Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, ameiagiza Halmashauri ya Manispaa ya Singida kuharakisha utekelezaji wa kulibadilisha matumizi dampo la Manga lililopo kijiji cha Mtipa kandokando ya barabara kuu ya Singida-Mwanza kuwa eneo la maegesho ya malori na kujenga hoteli na migahawa.
Akizungumza baada ya kutembelea dampo hilo, alisema eneo hilo yatakapojengwa maegesho, hoteli na vituo vya mafuta kitakuwa chanzo kizuri cha mapato ya Manispaa ya Singida kwa kuwa magari yatatoa ushuru na watu watakaowekeza hapo watatoa kodi.
Aidha, Serukamba ameziagiza Wilaya zote kuanza mkakati wa kupanda miti kandokando ya barabara na kufanya usafi kila siku ya Jumamosi kuanzia mwakani ili kutunza mazingira na kupendezesha miji.
Naye Meya wa Manispaa ya Singida, Yagi Kiaratu, amesema maelekezo ya Mkuu wa Mkoa wa Singida yatazingatiwa na kwamba Manispaa ilikuwa imeshaanza kubadilisha matumizi ya dampo la Manga.
Amesema dampo hilo wakati linaanzishwa mji wa Singida ulikuwa haujapanuka lakini baada ya mji kupanuka hivyo limetafutwa eneo la Mwankonko nje kidogo ya mji ambalo limeanza kutumika kama dampo jipya.
"Mpango wa Manispaa eneo lote la dampo la Manga litapimwa kujua ukubwa wake na baadaye itapitishwa michoro inayokidhi eneo hilo na baada ya hapo tutajenga hoteli, nyumba za kulala wageni, maegesho ya magari pamoja na eneo la mama lishe ili wanaoegesha magari yao waweze kupata huduma," Kiaratu amesema.
Kiaratu amesema kwamba Manispaa ya Singida itashughulika na suala la ujenzi wa maegesho ya magari lakini huduma nyingine zitafanywa na wawekezaji watakaopewa eneo hilo kuwekeza.
Aliongeza kuwa sheria ndogo za Manispaa zilizopo zitahuishwa zianze kutumika haraka na atakayepatikana akitupa taka ovyo atakamatwa na kutozwa faini kati ya Sh. 50,000 hadi 300,000.
Meya alisema Manispaa itaanza kuvitumia vikundi kazi vilivyo kila mtaa kwa ajili kukamata watu wanaochafua mazingira ili wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.
MWISHO
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.