MKUU wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba amewahimiza Watendaji wa kila Halmashauri kuhakikisha wanasimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa Mkoani humo ili iweze kuishi kwa wakati.
Serukakamba ametoa maagizo hayo leo (tarehe 25 Oktoba, 2023) wakati wa ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya sekta ya afya na elimu pamoja na kusikiliza changamoto za wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida na Manispaa na kuhimiza Watumishi hasa Wahandisi kuhakikisha wanasimamia miradi na kuijenga kwa kiwango cha ubora kulingana na thamani ya fedha zinazotolewa na Serikali.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa licha ya kuridhishwa na miradi ya ujenzi wa vituo vya afya lakini amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri hizo pamoja na Wahandisi wa Mkoa wa Singida kuhakikisha wanatembelea miradi pamoja na kuangalia mipango kazi ya Wakandarasi ili kuharakisha utekelezaji wa ujenzi wa miradi hiyo.
Amesema kuwa Mkoa wa Singida ni kati ya Mkoa ambao unapokea fedha nyingi za maendeleo hivyo kuna kila sababu ya kusimamia miradi hiyo na kuimaliza kwa wakati uliopangwa kwa ajili ya kuanza kutumiwa na Wananchi.
Kutokana na hali hiyo amemwagiza Mhandisi wa Mkoa kuhakikisha anatembelea miradi yote na kuikagua ili kujiridhisha na utendaji wa mafundi na kueleza kuwa Mkandarasi ambaye ataonekana kuwa siyo mwaminifu asitishiwe mkataba wake na kupewa kazi Mkandarasi mwingine ambaye ataonesha kuwa ni mwaminifu.
Amesema kuwa kwa sasa miradi mbalimbali ya maendeleo Mkoani humo ikiwemo Afya, Elimu, Maji, Miundombinu ya Barabara, nishati ya Umeme pamoja na Sekta ya Kilimo inaendelea vizuri na kwa kasi sambamba na kiwango bora kwa kuzingatia thamani ya fedha.
Akizungumzia miradi ya Sekta ya Elimu, amesema kuwa inatakiwa kukamilika ndani ya mwezi wa Desemba mwaka huu ili ifikapo Januari mwaka kesho watoto wanaoanza kidato cha kwanza wakute miundombinu yote imekamilika.
Hata hivyo amesema anataraji kuanza ziara ya kutembelea kila aina ya mradi unaotekelezwa katika halmashauri zote za Wilaya Mkoani humo kwa kuhakikisha anatembelea kila mradi bila ya kuchaguliwa ni mradi gani aende.
“Nimepanga baada ya wiki moja ijayo nitatembelea Wilaya zote za Mkoa wa Singida na kufika kwenye kila mradi ili niweze kujionea utendaji wa miradi hiyo na sitahitaji kupangiwa ni mradi gani wa kutembelea, kwa kufanya hivyo nitaweza kutambua ni wapi ambapo wanakwama au wanafanya vizuri” RC Serukamba.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.