MKUU wa Mkoa Singida, Peter Serukamba, amehitimisha ziara yake ya siku mbili kwa kutembelea miradi 30 katika Wilaya ya Iramba na kutoa agizo mahsusi kwa viongozi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kuhakikisha ifikapo Juni 20 mwaka huu iwe imekamilika ili fedha zisije zikarudishwa serikalini.
Akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Kyala leo (Mei 17, 2023) ambako alizindua mradi wa umeme uliotekelezwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) na kufanya majumuisho ya ziara yake, amesema hataki kuona fedha zilizoletwa na Serikali Kuu katika mkoa huu kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo zinarudi serikalini baada ya mwaka wa fedha kumalizika.
"Ifikapo Juni 30 Serikali huwa inachukua fedha ambazo hazijatumika, sisi wakuu wa mikoa tunayo maelekezo mahsusi kutoka kwa Waziri Ofisi ya RAIS, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) tunahakikisha fedha hizi hazirudi maana yake tuhakikishe miradi hii inatekelezwa," alisema.
Serukamba amesema katika ziara yake wilayani Iramba amejifunza upande wa Halmashauri na Serikali watendaji wanatakiwa kuisimamia kwa karibu sana miradi inayotekelezwa badala ya kuwaachia walimu na wananchi pekee yao waisimamie.
"Kwenye 'project management' lazima muwe na 'culture' ya kusimamia miradi hii kwani Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo hivyo itakuwa jambo la ajabu tusiposimamia tukaacha isikamilike kwa wakati," amesema.
Aidha, Mkuu wa Mkoa aliwahimiza wananchi kutunza miundombinu ya umeme na kulipa ankala kila mwezi ili kuiwezesha Wakala wa Umeme Vijijini (REA) pamoja na Shirika la Ugavi Umeme Nchini (TANESCO) ziendelee kutoa uduma bora na za uhakika kwa wananchi.
Katika miradi 12 aliyoitembelea leo Mkuu wa Mkoa hakuridhishwa na kasi ya ujenzi shule mpya za msingi za Kibululu na Nselembwe na kuwaagiza walimu wakuu wa shule hizo wanapobaini mafundi kama ndio kikwazo wasisite kuwaondoa na kuweka wengine.
Aliwataka madiwani, viongozi wa vijiji na kata kuwahamasisha wananchi waweze kushiriki katika ujenzi wa miradi hiyo.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Gunna Maziku, alimhakikishia Mkuu wa Mkoa kwamba yeye na viongozi wenzake watahakikisha wanaisimamia miradi hiyo na kukamilika ifikapo Juni 20 mwaka huu kama alivyotoa maelekezo.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.